Serikali imesema hadi kufikia sasa utekelezaji wa kufunga mtandao wa Wi-Fi katika maeneo ya umma umefanyika katika vituo sita nchini ambavyo vitatoa huduma ya internet za wazi (internet hotspot) ikiwa ni lengo la Serikali kuanzisha huduma za intaneti ya kasi katika maeneo yote ya umma.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Janeth Mahawanga jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano ya Habari, Kundo Mathew amesema Serikali imejipanga kufikisha huduma hiyo katika maeneo 20 ikiwemo hospitali, taasisi za elimu na vituo vya usafiri.
“Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tumejipanga kwa ajili ya kufikisha huduma ya intaneti ya Wi-Fi katika maeneo 20 na tutaendelea kufanya hivyo mpaka tutakapofikia lengo la Serikali ambalo ni kufikia asilimia 40 mwaka 2025,” amesema.
Ameyataja maeneo sita yaliyofungwa huduma hiyo kuwa ni Stendi ya Nanenane (Dodoma), Buhongwa (Mwanza), Kiembe Samaki (Unguja), Chuo Kikuu cha Dodoma Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu Saivu, Soko la Tabora na Chuo cha Ustawi wa Jamii (Rungemba).