Dodoma. Serikali imefungia tovuti 334, akaunti za Facebook 361, Instagram 12, Twitter 12 na vikoa 2,456 ambazo zilikuwa zinajihusisha na matangazo ya ukiukwaji wa maadili ikiwemo mapenzi ya jinsi moja.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatatu April 17, 2023 na Waziri wa Habari, Nape Nauye wakati akitoa nyengoza ya majibu ya Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ambaye amehoji mkakati upi wa Serikali kuhusu watu wanaohamasisha uvunjifu huo wa maadili.
Nape amesema serikali ilishadhibiti vitendo hivyo ikiwemo kuzuia matangazo kwenye vyombo vya habari lakini akasema kumekuwa na changamoto kwenye mitandao ya kijamii ambako nako wameanza kudhibiti.
Awali, mbunge huyo alihoji kuhusu sheria za Tanzania zinasema nini kuhusu masuala ya jinsi moja na kwenye swali la nyongeza akaomba ni kwa nini sheria hizo zisipelekwe bungeni ili kufanyiwa maboresho kwa lengo la kuwashitaki wote wenye dalili za kujihusisha na vitendo hivyo.
Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul amesema Serikali ya Tanzania haitambui mapenzi ya jinsi moja na kwamba imekuwa ikipiga vita vitendo hivyo katika maeneo mengi.
Gekul amesema sheria iko wazi kwamba, mtu akikutwa na makosa ya aina hiyo huchukuliwa hatua na kupewa adhabu ambayo yake ni kifungo cha maisha au miaka 30 gerezani.
Hata hivyo Naibu Waziri amesema jukumu la kulinda maadili ya Tanzania siyo la Serikali pekee bali wananchi wote wanatakiwa kulinda maadili kwa ushirikiano wa pamoja.
By Habel Chidawali
Mwandishi wa Habari