Moshi. Mtuhumiwa wa mauaji ya mke wake, Anthony Assenga, ametoa mpya katika Mahakama Kuu kanda ya Moshi, baada ya kufutiwa mashtaka kwa kitendo chake cha kumwamkia shikamoo jaji alipomuuliza kama aliua au la.
Hukumu hiyo dhidi ya Assenga, mkazi wa Mashati wilayani Rombo, ilitolewa Machi 31, mwaka huu na Jaji Juliana Masabo wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi na nakala ya hukumu yake kupatikana jana katika mtandao wa Mahakama Kuu wa TanzLii.
Awali, Ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa Februari 12, 2021 katika kijiji cha Mrere wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, alimuua kwa makusudi mkewe aliyetajwa kuwa ni Happiness Nyerere kwa kumkata kwenye koromeo kwa kitu chenye ncha kali.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipoitwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH) Februari 12,2022 na mshitakiwa huyo kusomewa na kuelezwa kosa lake na kutakiwa kujibu kama ni kweli alitenda kosa hilo ama la, mshitakiwa akajibu kwa neno; “Shikamoo.”
Mawakili waliokuwa wakimtetea, Lydia Mongi aliibua hoja ya uwendawazimu wa mshitakiwa na kuiomba mahakama itumie mamlaka iliyonayo na kuamuru mshitakiwa apelekwe Taasisi ya wagonjwa wa akili ya Isanga ili aweze kuchunguzwa akili.
Hoja hiyo haikupingwa na upande wa mashitaka na mshitakiwa alipelekwa Isanga Aprili 6,2022 na ripoti kutoka kwa daktari aliyemchunguza imeonyesha mshitakiwa alikuwa akisumbuliwa na wendawazimu na matatizo ya kisaikolojia kutokana na ulevi.
Baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, Machi 31,2023 Mahakama iliruhusu upande wa mashitaka uite mashahidi wake na iliita mashahidi wawili ambao ni askari polisi G.2392 Koplo Issack na aliyekuwa mpelelezi wa shauri hilo la mauaji, Elisante Mlanga.
Ilivyokuwa
Katika ushahidi wake, Koplo Issack aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio alipokea taarifa kutoka kwa mkuu wa kituo (OCS) kuwa kuna mauaji yametokea na alikwenda eneo la tukio na kumkuta marehemu amelala kitandani na jeraha kwenye koo.
“Yeye na maofisa wengine waliuchunguza mwili na kubaini ulikuwa na jeraha kwenye koo ambalo liliashiria kuwa marehemu alikuwa amekatwa na kitu chenye ncha kali,” inaeleza sehemu ya hukumu hiyo ya Jaji Masabo aliyoitoa Ijumaa iliyopita.
“Walipouliza kuhusu kiini cha mauaji hayo, kaka wa mtuhumiwa aliwaambia (askari) kwamba mshitakiwa hana akili timamu. Kuna wakati hufanya vitu kama mwendawazimu na kutishia kukata watu kwa panga,”anaeleza Jaji Masabo.
Wakati wanakagua tukio hilo, ilibainika mtuhumiwa alikuwa ameshajisalimisha kituo cha Polisi Mashati wilayani Rombo ambapo alitoa taarifa kuwa alikuwa ameua jambazi.
Shahidi wa pili, Mlanga, yeye aliiambia mahakama kuwa walijaribu kufanya mahojiano na mtuhumiwa, lakini yalishindikana kukamilika kwa kuwa tabia za ajabu ajabu za mtuhumiwa na wakati mahojiano yakiendelea alipanda juu ya meza.
Alichokisema Jaji Masabo
Katika hukumu hiyo, Jaji Masabo alisema baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa afya ya akili kama ilivyo kwa mshitakiwa, sheria inaelekeza mahakama kujiridhisha na ripoti na kama kweli mshitakiwa alipotenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
Jaji Masabo alisema baada ya kuipitia kwa umakini ripoti hiyo ya Taasisi ya Isanga na ushahidi wa mashahidi hao wawili, imethibitika vizuri kuwa mshitakiwa alikuwa na mienendo isiyo ya kawaida, jambo linaloashiria hakuwa na utimamu wa akili.
“Kwa mtazamo wangu thabiti, ushahidi wao umethibitisha ipasavyo ripoti ya kitabibu kwamba mshtakiwa alikuwa kichaa wakati anatenda kosa. Kwa hiyo mahakama imeona ni kutokana na ukichaa wake mshitakiwa alifanya kitendo hicho,”alisema Jaji Masabo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 219(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Jaji aliamuru Assenga ahamishiwe na kuhifadhiwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili kama mgonjwa mwenye kichaa jinai (criminal lunatic) na ashughulikiwe kulingana na sheria.