BAADA ya kumalizana dhidi ya Wydad Casablanca ya nchini Morocco usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ sasa nguvu na akili zake sasa amezihamishia kwa wapinzani wake Yanga na Azam FC.
Simba jana usiku walitarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mohammed V, ulio Mji wa Casablanca nchini Morocco kuvaana dhidi ya Wydad Casablanca.
Timu hizo zilicheza katika mchezo wa mkondo wa pili wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliochezwa wiki moja iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam, Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Jean Baleke.
Simba wapo katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 63 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara wanapambania taji hilo na Yanga ambao ndio watetezi walio kileleni wenye pointi 68.
Pia Simba wana kibarua kigumu dhidi ya Azam FC watakaovaana hivi karibuni katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la FA msimu huu.
Simba inatarajiwa kurejea na nguvu zote katika ligi na FA baada ya kutoka kucheza dhidi ya Wydad Casablanca ili kuhakikisha wanabeba mataji yote hayo wanayoshindania dhidi ya Yanga na Azam FC.
Robertinho hivi karibuni alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Katika msimu huu ni lazima tuchukue makombe au moja kati ya haya tunayoshindania ili kuwapa furaha mashabiki wetu furaha.
“Wakati nakabidhiwa jukumu la kuifundisha Simba, niliomba muda wa kuitengeneza, nashukuru nikaaminiwa na kupewa, tayari timu inaanza kuonekana inacheza soka safi.
“Lakini bado ninahitaji muda zaidi ya kuendelea kutengeneza timu, nashukuru hivi sasa muunganiko umeanza kuelewana wa wachezaji wangu,” alisema Robertinho.
STORI NA WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI JUMAMOSI