Mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga inaendelea kuwatoa watu jasho kila mmoja akielezea hali ya mchezo huo itakavyokuwa huku nahodha wa zamani wa timu hizo, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ akisema; “Sio ajabu mtu akala za kutosha.”
Simba na Yanga zinakutana katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara msimu huu, likiwa pambano la 110 tangu Ligi ya Bara ilipoasisiwa mwaka 1965, huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Yanga ndio mtetezi na kinara wa ligi hiyo ikiwa na pointi 68, ikifuatiwa na Simba yenye 60, huku kila timu ikicheza mechi 25 na kwenye pambano la kwanza lililopigwa Oktoba 23, mwaka jana zilishindwa kufungana kwa kutoka 7Timu hizo zinakutana zikiwa zimetoka kupata matokeo kwenye mechi zilizopita za ligi, Yanga ikiifumua Kagera Sugar kwa mabao 5- 0, wakati Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Ihefu.
Beki huyo wa kati wa zamani aliyeng’ara pia Ushirika Moshi, Majimaji na Taifa Stars, alisema kwa sasa Yanga ni timu bora, lakini Simba ina wachezaji imara hivyo kama mmojawapo atakosea popote anaweza kujikuta akila nyingi na kuwaacha na mshangao.
“Mfano kuna mechi moja nikiwa Yanga tulikuwa na kikosi bora, lakini sijui ilikuwaje, Simba ikatufunga 4-1 na nilijikuta nikipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Dua Said, tulipaniki sana,” alisema Gari Kubwa anayeishi kwa sasa Kyela, Mbeya na kuongeza;
“Kwa maana hiyo mechi ya Jumapili sijaona kama nani atashinda ila nafikiri kuna mtu atakula nyingi, Yanga ni bora ambapo yeyote anaweza kufunga bao na Simba ina wachezaji wazuri kama Jean Baleke ambaye anaweza kufanya lolote muda wowote, “alisema staa huyo.
Beki huyo aliyewahi kutesa na Taifa Stars, aliongeza kuwa mechi nyingi za watani ni kama huchezwa zaidi nje ya uwanja hivyo anaye muwahi mwenzake ndiye hunufaika na kusisitiza kuwa mchezo huo hakuna sare.