Tunashindwa Kusema Ukweli Kuhusu Nabi, Yanga Yake ni Bora zaidi Kuwahi Kutokea

 


Watu wa soka nchi hii ni wataalamu wa majungu na mizengwe. Wanapenda zaidi kuona mabaya kuliko mema.


Ndio maana ni rahisi zaidi kwa habari mbaya nchini kutembea kuliko nzuri. Watu wanapenda zaidi kuona kasoro.


Ndio sababu ni rahisi kuziona habari nyingi za sakata la Fei Toto kuliko sifa za Fiston Mayele anayeibeba Yanga mgongoni mwake kila siku.


Ni rahisi mtu kumkosoa Stephane Aziz Ki kwa kucheza vibaya kuliko kusifu kiwango bora cha Djigui Diara pale Yanga.


Ndio watu tulionao. Tutafanya nini. Ni kuvumiliana tu kama watu wa Dar es Salaam wanavyovumilia joto kali.


Kasumba hii imesababisha tunashindwa kuzungumza ukweli kuhusu Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi. Tunaona kama kazi anayoifanya pale Yanga ni ya kawaida.


Nadhani baada ya Hans Van Pluijm, Yanga imepata kocha mwingine bora zaidi. Pluijm aliifanya Yanga kuwa hatari.


Yanga ilicheza vizuri kwenye mechi za ndani na kimataifa. Ni kocha bora kuwahi kutokea ndani ya klabu hiyo kongwe nchini na barani Afrika.


Ni katika nyakati zake Yanga ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza. Ikiwa ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kufanya hivyo tangu michuano hiyo ilivyobadilishwa mwaka 2004. Yanga ilicheza hatua hiyo mwaka 2016. Inafurahisha sana.


Baada ya miaka kadhaa Yanga sasa imekuwa na Nabi. Amebadili kila kitu pale Jangwani. Yanga inacheza soka la kuvutia.


Alianza kama utani. Akamaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote na kuipa Yanga taji la kwanza ndani ya miaka mitano. Nani anajali? Hakuna.


Tunapenda zaidi kuzungumza mabaya kuliko mazuri. Yanga ya Nabi imeendelea kuweka rekodi nyingi Ligi Kuu Bara.


Msimu huu imepoteza mchezo mmoja tu. Ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa - tena kwa kishindo kikubwa.


Nabi ameipeleka Yanga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.


Tena kwa rekodi ya kupata ushindi ugenini dhidi ya Club Africain ya Tunisia. Ni jambo la kusisimua sana.


Uzuri ni kwamba katika kundi lake Yanga inacheza soka la kuvutia sana. Inatawala mechi inazocheza hapa nyumbani na ugenini.


Mfano mchezo dhidi ya US Monastir ya Tunisia. Licha ya kupoteza kwa mabao 2-0, Yanga ilicheza soka safi sana. Ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na kuwapa presha kubwa wenyeji.


Tazama walichofanya dhidi ya TP Mazembe kwa Mkapa. Mazembe sio tu ilifungwa, lakini na mpira mwingi ulipigwa pale kwa Mkapa. Hii ndio Yanga ya Nabi. Inavutia kutazama.


Kocha huyu raia wa Tunisia amefanikiwa zaidi kutengeneza timu kimbinu na kiufundi. Akajitahidi kupata ubora wa kila mchezaji katika nafasi yake.


Amekuwa na uchaguzi mpana katika kila eneo. Mfano ana mabeki bora watatu wa pembeni. Ana Joyce Lomalisa, Kibwana Shomary na Djuma Shaban. Hawa wanampa uhuru katika falsafa yake. Wanaongezeka kushambulia muda mwingi.


Katika kiungo ana utajiri mkubwa na wote wakicheza unapata ladha ileile. Ni ngumu kuona pengo la mchezaji mmoja.


Ndio sababu Bernard Morrison hajacheza kwa miezi mitatu sasa na hakuna anayejali. Timu inacheza vizuri kila siku. Ni ngumu watu kumkumbuka aliyeko nje.


Watu waache kumsifia Clement Mzize waanze kumkumbuka mtukutu Morrison? Sio kwa Yanga ya Nabi. Ameitengeneza vyema Yanga.


Siku akiondoka Yanga tutamkumbuka na kukiri ubora huu ambao leo watu wamekaa kimya hawausemi.


Ni kama yule Sven Vanderbroek alivyoondoka pale Simba. Watu walikuwa wakimuona kama kocha wa kawaida, lakini baada ya kuondoka ukweli ukajulikana.


Na hii ndio inayonifanya kuamini kivuli cha Nabi hakionekani leo, lakini kitakumbukwa pale atakapoondoka Jangwani kama ambavyo Yanga ilivyoteseka baada ya Pluijm kuondoka na ufundi wake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad