Ule Moshi Waiponza Wydad CAF...Washitakiwa na Simba, Kumbe Waliruka na Kuvamia VIP



Ule Moshi Waiponza Wydad CAF...Washitakiwa na Simba, Kumbe Waliruka na Kuvamia VIP

SIMBA inataka kurudia maajabu yake ya kumtupa nje bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa CAF ambao ni Wydad Athletic Club, lakini kabla ya mechi ya pili tayari imeandaa malalamiko juu ya mashabiki wa timu hiyo.

Simba juzi ilipata ushindi wa bao 1-0 na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa itafanya hivyo itakuwa mara yao ya pili kufika hatua hiyo.

Kabla ya kuondoka Simba leo itawasilisha rasmi malalamiko yao kwa Shirikisho la Soka Afrika Caf juu ya kutoa tahadhari za mashabiki wa Wydad kufuatia matukio waliyoyafanya kwenye Uwanja wa Mkapa dakika 10 za mwisho kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.

Kama hukuona ni kwamba mashabiki hao maarufu kama Ultras ambao wanahesabika kuwa na vurugu nyingi, waliruka uzio wa jukwaa na kutua jukwaa moja la VIP B bila ruhusa.

Hawa wamekuwa wakiambatana na timu hiyo kila mahali wanapokwenda na wanatajwa kuwa na vurugu kubwa kwenye mechi za ugenini kuliko nyumbani kwao.

“Hawa wanaitwa Ultras wapo kama 300 hivi ingawa sidhani kama pale wapo wote, wanakwenda na timu yao popote na wanashangilia mwanzo mwisho, shida wanafujo sana,” alisema shabiki mmoja wa Wydad wakati mechi inaendelea.

Baada ya kuruka uzio huo wakati timu yao ikishambuliwa kwa nguvu na Simba waliwasha fataki za moshi ambao uliwazuia mashabiki wengine kuona pamoja na wachezaji na waamuzi kuona giza hali iliyomfanya mwamuzi kusimamisha mchezo.

Msimu uliopita Simba iliwahi kukutana na kasheshe la mashabiki kama hao wa RS Berkane ya hapohapo Morocco kwa kuwasha fataki kama hizo na waliripoti kwa CAF kisha Berkane kupunguziwa idadi ya mashabiki kwenye mechi zao.

Mara baada ya mchezo wa juzi mabosi wa Simba tayari walishaanza hesabu hizo wakikusanya vielelezo vya picha za mnato na zile za video kwa lengo la kuziwakilisha CAF kwa idara ya mashindano hayo.

Simba inataka kujiweka katika mazingira salama kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Wydad ambao utachezwa nchini Morocco Aprili 28, saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Meneja wa Habari wa Simba Ahmed Ally amelithibitishia Mwanaspoti kuwa watawasilisha barua rasmi kwa CAF leo katika kuweka tahadhari ya mashabiki hao ili wasiiharibu saikolojia ya wachezaji wao.

“Simba ina mashabiki Morocco ambao tutawakuta kule,t uliwakuta pia tulipocheza dhidi ya Raja kama walifanya vitendo hivi ugenini hawatashindwa kufanya wakiwa kwao tahadhari yetu ipo hapo,”alisema Ahmed.

“Tutakutana Jumatatu kumalizia hilo nadhani kwa waliokuwa uwanjani jana (juzi), waliona kilichofanyika ilikuwa huwezi kuona mbele na mbaya zaidi walifanya yale wakati tunatafuta bao la pili, tutawaambia Caf kila kitu ingawa tunafahamu nao viongozi wao walikuwa hapa wameona.”

Hatua mbaya kwa Wydad ni kwamba mratibu wa mchezo huo Joshua Knipp raia wa Afrika Kusini ndiye aliyesimamia mchezo wa Berkane dhidi ya Simba ambapo juzi alikuwa tena kazini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

ROBERTINHO ANAJIPANGA

Wakati mabosi wakijipanga hivyo kocha wao naye Robert Oliveira ‘Robertinho’ anapasua kichwa jinsi ya kuwavamia wapinzani wao katika safari yao ambayo huenda ikaanza kesho Aprili 25, kuwafuata Wydad.

Robertinho ameliambia SOKA LA BONGO kuwa kwa sasa anataka kufanya maamuzi ya mifumo miwili migumu itakayokwenda kuwapa nguvu kwenye mchezo wa ugenini huku akichimba mkwara kwamba Simba iheshimiwe sasa.

“Tunataka kuhakikisha tunawaweka katika wakati mgumu licha ya kucheza kwao,nawaamini wachezaji wangu sitaki turudie makosa haya ambayo kwetu yalishapita,” alisema Robertinho raia wa Brazil.

“Sisi sio timu nyepesi tena watu watuheshimu tunaweza kwenda ugenini na tukafanya kitu, tunawaheshimu Wydad lakini hatutakwenda kinyonge pale Casablanca tutakwenda kupigania heshima ya klabu hii kubwa.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad