Kama Ufaransa wana Kyllian Mbappe, Hispania wana Karim Benzema na England wana Earling Halaand, basi Tanzania tumebahatika sana. Sisi tuna Fiston Mayele na Jean Baleke. Tuna wanaume wawili wenye uwezo mkubwa wa kutupia mpira wavuni.
Baada ya siasa zote za Cezar Manzoki hatimaye Simba wamejitafuta na kujipata. Mechi 14 tangu Baleke ajiunge na Simba mabao 14 katupia kambani. Huyu ndiye mshambuliaji waliyekuwa wanamtafuta.
Huyu ndiye kiumbe anayetakiwa kuongoza jahazi kwenye safari ya kumuua Wydad Casablanca. Moja kati ya vitu wanavyokosa wachezaji wetu wengi ni kutokuwa na mwendelezo.
Mechi mbili zilizopita Baleke amefunga mabao matano. Sio jambo dogo. Ni mara chache tumekuwa na wachezaji wa daraja hili kwenye ligi yetu. Kufunga mabao 14 kwenye mechi 14 tangu atue Simba huyu ni Halaand mtupu!
Moses Phiri alianza kwa kasi sana, lakini baada ya kuumia,ni kama ameanza upya kujitafuta.Simba wa msimu huu wanaweza wasiwe na ubora kama ule wa kina Luis Miquessone na Lary Bwalya, lakini tusiwachukulie poa. Wanaonekana kutaka kumaliza msimu kwa kishindo. Wanaonekana wanataka kutengeneza heshima. Hakuna presha yotote kwenye kikosi. Jean Baleke ana faida kubwa moja tu kwa Simba ya msimu huu kila mtu anatengeneza nafasi za kufunga.
Simba ndiyo timu pekee yenye wapishi bora wa mabao zaidi ya watano. Kila mtu pale Simba anatengeneza nafasi za kufunga. Kama Baleke hataanza kupelekwa kwenye sauna za Sinza kukandwa mwili. Kama Baleke hatapelekwa kwa kinadada wale wa Magomeni Mapipa ana kitu. Atafika mbali sana. Kama Baleke hatapelekwa Wavuvi Kempu na Kitambaa Cheupe kila siku atafunga sana. Ukitazama namba za Baleke unaogopa. Ni mtu kazi hasa.
Simba walihitaji mtu wa namna hii. Unapokuwa na viungo washambuliaji kama Clatous Chama na Said Ntibazonkiza unahitaji mjuba mmoja tu wa kusimama pale juu kama komando wa kutupia. Baleke amezungukwa na mafundi watupu. Akiwa na nidhamu ya kwenda Wavuvi Kempu na Kitambaa Cheupe huku akikumbuka wajibu wake ataweka mipira mingi sana kabatini.
Jean Baleke ni Halaand mtupu. Mabao 14 ndani ya mechi 14. Moja kati ya vitu vinavyosubiriwa kwake ni mwendelezo wa namba hizo. Tofauti kubwa kati ya Baleke na Mayele ni mwendelezo. Mayele tayari ameshaonyesha umaridadi wa kufumania nyavu. Amefunga halafu akafunga tena. Baleke bado anadaiwa. Wacha tuone msimu huu anamalizaje. Wacha tuone msimu huu anaipeleka wapi Simba. Kwa aina ya wachezaji wanaomzunguka pale Simba anatakiwa kutupia sana kambani.
Sasa ni muda wa Simba kuachana na zile porojo za Cesar Manzoki. Sasa ni muda wa kuachana na siasa za uchaguzi. Ni muda wa miguu ya Baleke kuongea. Ni muda wa kuitafuta nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Cesar Manzoki amekuwa mchezaji anayetumika sana kisiasa pale Msimbazi. Mashabiki na wapenzi wa soka wametaniwa sana na kuchezewa akili kwamba anakuja, lakini hakuna kitu. Kumbe mshambuliaji hatari alikuwa DR Congo. Kumbe mtambo wa mabao upo hapo TP Mazembe. Huu ni muda wa Baleke kuongea na wana Simba. Huu ni muda wa Baleke kuwapa furaha wana Msimbazi. Miguu ya dhahabu. Mtambo wa mabao. Simba sasa ipo kwenye mikono salama.
Ntibazonkiza na Chama kazi yao sasa ni moja tu - kuisogeza kidogo mipira ndani ya boksi. Mnyama bado msimu haujaisha kwake. Bado ana deni kwa mashabiki wake. Kuna kila dalili za kukosa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, lakini bado kuna vita ya kupigana.
Kuna Kombe la Azam Sports na la Ligi ya Mabingwa Afrika. Huku bado uwanja uko wazi. Msimu bado haujaridhika. Ubingwa wa Afrika bado unaonekana ni ndoto za mchana kwa timu za Tanzania, lakini mpira wakati mwingine huwa unatupa matokeo ya ajabu sana. Kombe la Shirikisho la Azam bado milango iko wazi kwa Mnyama. Ni Baleke tu kuendelea kutupia kambani mipira.
Ni vigumu kubeba ubingwa wa ligi kwa sababu wameachwa na Yanga iliyo bora pia, lakini Kombe la Shirikisho wanaweza kushinda. Ni ngumu kupata ubingwa wa Afrika lakini nusu fainali milango iko wazi.
Unahitaji watu kama kina Baleke kuwamaliza Wydad Casablanca ndani ya Dar es Salaam. Unahitaji kumchinja Mwarabu mabao matatu kwa Mkapa. Unahitaji kumpiga wiki kwa Mkapa. Kwa moto huu wa Baleke, Chama na Ntibazonkiza msimu bado haujamalizika kwa Simba. Bado kuna jambo halijakamilika. Bado nayaona mabao mengi kwa Baleke. Bado naiona kumbukumbu nzuri kwa Mnyama msimu huu. Huyu Baleke ni Halaand mtupu kwenye ligi yetu.