Dodoma. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Festo Dugange amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali ya gari.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi limezipata, zinaeleza Dk Dugange alipata ajali hiyo usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023. Hata hivyo, mpaka sasa si Jeshi la Polisi wala viongozi wa wizara yake waliokuwa tayari kuthibitisha kuhusua ajali ya kiongozi huyo.
Licha ya jitihada za Mwananchi kuwatafuta Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki na Naibu wake, Deo Ndejembi pamoja na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa lakini, hakuna aliyekuwa tayari kuzungumzia taarifa hizo.
Hata hivyo, akihutubia wananchi wa Wilaya ya Chamwino, Dodoma kwenye uzinduzi wa majengo ya Jeshi la Zimamoto Aprili 26, 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia mbunge wao Ndejembi hakuhudhuria hafla hiyo kwa sababu alipewa jukumu la kumuuguza naibu waziri mwenzake aliyepata ajali.
"Ndugu wananchi, naleta salamu nyingi kutoka kwa mbunge wenu Ndejembi (Deo) alitamani kuwa nanyi hapa, lakini tumempa jukumu la kuangalia matibabu ya naibu waziri mwenzake alipata ajali Jana," alisema Majaliwa bila kumtaja naibu waziri huyo aliyepata ajali.
Taarifa za uhakika ambazo Mwananchi limezipata kutoka hospitalini hapo, zinaeleza Dk Dugange ambaye ni mbunge wa Wanging’ombe, mkoani Njombe alifikishwa hospitalini akiwa mahututi na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.
"Ni kweli majeruhi tuliyenaye ni Dk Dugange, alifikishwa hapa akiwa kwenye hali mbaya lakini tunamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea vema," kilisema chanzo chetu.
By Habel Chidawali
Mwandishi wa Habari
Mwananchi