CAG Charles Kichere
UKAGUZI uliofanywa na Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG), umebaini hadi kufikia Juni 30, 2022 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ilikuwa na waidhinishaji wa akaunti 12 za benki, ambao hawakuwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo, baada ya kuhamishiwa kwenye taasisi zingine za serikali.
“Ni maoni yangu kuwa mapungufu yaliyobainika yanatokana na ukosefu wa mipango ya usimamizi ya kuteua waidhinishaji wa akaunti kwa wakati, hivyo kuongeza hatari ya wafanyakazi wasio wa Mamlaka ya Bandari kutoa fedha bila kujulikana na kuidhishwa na mamlaka.
“Ninapendekeza kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania ihakikishe benki zote zina waidhinishaji waliothibitishwa kuwa ni wafanyakazi wa mamlaka hiyo na kuwajulisha benki mara moja kuhusu mabadiliko yanayohusiana na waidhinishaji wa akaunti za benki,” amesema CAG Charles Kichere.
Kichere ameyabainisha hayo jijini Dodoma jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa za ukaguzi bungeni kwa hesabu za mwaka 2021/22.