Yanga: Tumepokea ofa tatu za Fei Toto, tunamtakia kila la heri!






 Klabu ya Yanga imesema mpaka sasa imepokea ofa kutoka kwenye vilabu vitatu vya soka kwa ajili ya kutaka huduma ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ambaye ana mgogoro na klabu hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu ya Yanga, Wakili Patrick Simon wakati akifanya mahojiano maalum na Yanga TV kuhusu sakata la mchezaji huyo na klabu yake ambapo ameshaomba TFF ivunje mkataba wake na Yanga kwa kile anachodai kuwa hana furaha ndani ya timu na ananyanyaswa.


"Klabu mpaka sasa imepokea ofa kadhaa kuhusu kumtaka Feisal, lakini huwezi kuja moja kwa moja kwa klabu wakati hujui mchezaji yuko wapi. Kwa hiyo ofa ni kweli zipo na sisi tumewashauri walioleta ofa kuwa mchezaji hayuko na sisi na hajawa na sisi muda mrefu.

"Kwa hiyo wamfuate mchezaji, wakubaliane naye makubaliano binafsi, kisha watakuja kwetu nasi tutawapa ofa yetu, tukikubaliana tutakuwa tayari kumwachia.

"Naomba watu wajue kwamba sisi hatujamng’ang’ania Fei Toto. Baada ya maamuzi ya TFF, Yanga ilitoa msimamo, Fei akitaka kurudi kulinda kipaji chake, sisi tunamkaribisha. Fei akitaka kuendelea kucheza na Yanga, hela yoyote akitaka tupo tayari kumpa, Yanga haina shida ya hela sasa hivi.

"Lakini pia hata akitaka kuondoka, aje mezani tumalizane naye vizuri, hata kama kuna klabu inamtaka waje, kama hivi sasa tumepokea ofa tatu mpaka sasa hivi, kwa hiyo wakikubaliana na mchezaji wakija kwetu tutamalizana.

"Sisi tunampenda Fei Toto na tunamheshimu, ametusaidia katika kipindi kirefu, tangu Yanga ya kipindi kile ikiwa haina chochote. Tunatamani awe sehemu ya mafanikio makubwa ya klabu yetu, lakini yeye mwenyewe kaamua kuondoka.

"Tunamtakia kila la kheri, lakini ajue hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya Timu, Yanga ilikuwepo tangu mwaka 1935 hata baba yaje alikuwa hajazaliwa, na Yanga itaendelea kuwepo hata baada yay eye kutokuwepo, lakini ajue Wanayanga wanataka aiheshimu klabu yake, afuate taratibu, nasi tutampa Baraka zetu," amesema Wakili Simon.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad