KESHO Jumapili Yanga watakuwa uwanjani nchini Nigeria kuhakikisha kuwa wanaendelea kuitetea heshima yao wakati watakapokuwa wakivaana na Rivers United kwenye mchezo mgumu.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na utakuwa ni muhimu kwa ajili ya kuweka heshima kwa timu zote mbili ambazo hazina rekodi yoyote kubwa kwenye michuano hii.
Katika timu zote nane ambazo zimetinga kwenye hatua hii, Yanga pamoja na timu nyingine sita hazina rekodi kubwa ikiwa ni tofauti na Pyramids na FA Rabat ambao wamewahi kuchukua ubingwa huu mara moja.
Kwenye michuano ya msimu huu timu nyingi ambazo ni vigogo kwenye Kombe la Shirikisho aidha zilitolewa kwenye hatua ya awali au zipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vinara ambao wanaongoza kwa kutwaa ubingwa huu CS Sfaxien ambao wameshatwaa mara tatu, hawapo kwenye hatua hii, lakini pia mabingwa watetezi Berkane ambao wameshatwaa ubingwa huu mara mbili hawapo hapa.
Hali hii inafanya michuano hii msimu huu kuwa wazi na timu yoyote ambayo inaweza kuchanga karata zake vizuri inaweza kufanikiwa kutwaa ubingwa huo na kujishindia kitita cha shilingi bilioni 2 na zaidi.
Rivers vs Yanga
Huu ni mchezo ambao kwa mashabiki wa soka hapa nchini wanausubiri kwa hamu kubwa kutokana na mwenendo wa Yanga kwa sasa kwenye ligi na michuano ya kimataifa.
Yanga baada ya kupangwa na Rivers ya Nigeria ambayo ilifuzu ikiwa imeshika nafasi ya pili kwenye Kundi B chini ya Asec Mimosas.
Kitakwimu Yanga wanaonekana kuwazidi Rivers kwenye sehemu kadhaa kubwa, jambo ambalo linaongeza hali ya hamasa kwenye timu hiyo, katika michezo sita ya hatua ya makundi Yanga wakiongoza Kundi D mbele ya Monastir walifanikiwa kukusanya pointi 13 zikiwa ni tatu mbele ya Rivers lakini timu zote zikafunga mabao tisa.
Yanga walionekana kuwa juu ya Rivers kwenye safu yao ya ulinzi ambapo wao waliruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne tu na Rivers wakifungwa mabao saba, tofauti hii inaonyesha kuwa Yanga wanaweza kupata mabao mengi kwenye mchezo huu lakini wakati huohuo wanaweza kuruhusu mabao machache tofauti na Rivers.
Katika michezo mitano ya mwisho iliyopita, Rivers wamefanikiwa kushinda mchezo mmoja tu, wakitoka sare miwili na kufungwa miwili lakini kwenye michezo hiyo wameruhusu mabao matano nao wamefunga mabao manne hali ambayo inaonyesha udhaifu wao kwenye maeneo yote mawili, ulinzi na ushambuliaji.
Kwa upande wa Yanga mambo yanaonekana kuwa tofauti huku takwimu zikiwabeba kwenye mchezo huu baada ya kufanikiwa kupata ushindi kwenye michezo yote mitano ya mwisho, wakiwa wamefanikiwa kufunga mabao 13 lakini kuonyesha kuwa wameendelea kuimarika kwenye eneo la ulinzi wameruhusu bao moja tu, kwa hapa nchini wakiweka rekodi ya kushinda michezo 12 mfululizo.
Hii inaonyesha utofauti mkubwa uliopo kwenye safu ya ushambuliaji na ulinzi kati ya Yanga na Rivers kwenye mchezo utakaopigwa Jumapili saa 1:00 kwenye Uwanja wa Yakubu Gowon nchini Nigeria.
Hata hivyo, bado pia kuna tofauti kubwa kwenye timu hizo kwenye upande wa thamani ya vikosi ambapo mtandao maarufu wa Transfer Market, unaonyesha kuwa kikosi cha Yanga kina thamani ya bilioni 5, lakini upande wa Rivers mambo ni tofauti ikionekana kuwa timu changa kwenye michuano ya kimataifa na ndiyo timu ambayo inatajwa na mtandao huo kuwa ina thamani ya chini zaidi kwenye hatua hii ikiwa na ukwasi wa milioni 580.
Kwenye upande wa chati ya wafungaji, wakati Yanga wakiwa na Fiston Mayele akiwa na mabao matatu kwenye michezo sita, wenyewe watakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha wanamzuia mshambuliaji wa Rivers, Paul Acquah ambaye ameshafunga mabao manne kwenye michuano hiyo hadi sasa.
Kwenye wastani wa umri kwa timu hizo zote ni miaka 26, zikionekana kuwa kwenye wakati sahihi wa mapambano huku Rivers wakiwa na wachezaji nane kutoka nje ya Nigeria na Yanga wakiwa na wachezaji 13 ambao wamesajiliwa kwenye michuano ya kimataifa kutoka nje ya Tanzania.
Ukiachana na mchezo huu wa River na Yanga, inaonekana kuwa kama Yanga wakipita kwenye hatua hii wanaweza kuwa na wakati mgumu kama watavaana na Pyramids au FAR Rabat ambazo zinaonekana kuwa na historia kubwa kwenye michuano hii.
Kwa timu zilizopo, Rabat wanaonekana kuwa kinara wakiwa walitwaa ubingwa huo mara moja mwaka 2005 na kufika fainali mara moja mwaka 2006 Wakiwa wanafuatiwa na Pyramids ambao walifanikiwa kufika fainali mara moja mwaka jana.
Timu zinazoongoza kuchukua Kombe la Shirikisho
CS Sfaxien 3
Étoile du Sahel 2
Berkane 2
TP Mazembe 2
Raja Casablanca 2
Nchi zinazoongoza kuchukua ubingwa
Morocco 7
Tunisia 5
Congo 2
Misri 2.