Dar es Salaam. Ndege ya Kampuni ya Frankfurt Zoological Society (FZS), imepata ajali katika kiwanja cha Ndege cha Matambwe, Hifadhi na Taifa ya Nyerere, Mkoa wa Morogoro na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi mmoja.
Rubani mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bernard Shayo kutoka FZS na Amani Mgogolo
Ajali hiyo imetokea leo Ijumaa Mei 18, 2023 saa 5:30 asubuhi wakati ndege hiyo aina ya Cessina 192 5H-FZS ikiruka kwenda katika doria ikiwa na abiria watatu na rubani mmoja.
Waliofariki papo hapo ni rubani mstaafu wa wizara ya maliasili na utalii, Bernard Shayo kutoka FZS na Amani Mgogolo huku Theonas Nota ambaye alikuwa Askari Mhifadhi amefikwa na mauti baada ya ndege iliyokuwa ikimkimbiza hospitali kutua Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.
Majeruhi ni Evanda Elisha, askari wa uhifadhi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) ambaye amejeruhiwa na anaendelea na matibabu.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya maliasili na utalii iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa wizara hiyo, John Mapepele ikimkunuu Katibu Mkuu wa wizara, Dk Hassan Abbas.
Katika taarifa hiyo, waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa ametuma salamu za pole kwa familia za watumishi hao.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akiwapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.