Kenya. Mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyekuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi cha Khwisero kilichopo Kaunti ya Kakamega nchini Kenya anadaiwa kubakwa na mmoja wa ofisa wa polisi wa kituo hicho.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko ya nchini humo imesema mwanafunzi huyo alikamatwa Aprili 28, mwaka huu akiwa na rafiki yake kwa kosa la kwenda kwa mtu anayesemekana ni mpenzi wake, hivyo wazazi wao wakawaomba polisi kuwakamata na kuwasweka mahabusu kama adhabu.
Wakiwa kituoni hapo askari alikwenda na kumtaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16, kumfuata kwenye chumba kingine ambapo alimuamuru avue nguo.
Mkurugenzi wa Huduma za Kijamii, Huduma za Watoto, Utamaduni na Jinsia wa kaunti hiyo, Vivian Ayuma amesema kuwa mtuhumiwa alimnajisi mtoto huyo kwa kutumia kinga (kondomu) ingawa bado hajakamatwa.
"Hili ni jambo la kusikitisha sana ambalo limefunikwa chini ya kapeti. Tunaomba uchunguzi kamili ufanyike kuhusu tukio hili la kusikitisha. Tunahitaji askari huyu afunguliwe mashtaka kwa kumsababishia binti maumivu na kuharibu maisha yake," amesema Ayuma.
Imeandaliwa na Sute Kamwelwe.