Aucho: Tulieni, Makombe Mengine Yanakuja Yanga



KIUNGO mkongwe mkabaji raia wa Uganda, Khalid Aucho amesema kuwa bado wana deni kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo, la kubeba makombe mawili ambayo yapo mbele yao kwa sasa.

Yanga tayari wametwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya juzi kutangazwa kuwa mabingwa baada ya kupata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Dodoma Jiji.

Timu hiyo, wamebakisha makombe mawili wanayoyashindania katika msimu huu ambayo ni Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika ambalo wamefuzu hatua ya Nusu Fainali na kesho watajitupa uwanjani kucheza mchezo wa pili dhidi ya Marumo Gallants.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam, Yanga walipata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Bernard Morrison na Stephane Aziz Ki.


Khalid Aucho
Akizungumza na Spoti Xtra, Aucho alisema kuwa binafsi yeye amepanga kuchukua makombe yote waliyoyabakisha katika msimu ambayo ni FA na shirikisho na hilo linawezekana kutokana na malengo ya viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki.

Aucho alisema kuwa anataka kuona akiwapa furaha mashabiki wa timu hiyo, kwa kuchukua makombe hayo yote mawili waliyoyabakisha baada ya kubeba la ligi, licha ya kuamini kuwepo ugumu wa upinzani.

Aliongeza kuwa ana furaha kubwa kutetea ubingwa wa ligi msimu huu, hali inayomfanya asijutie kujiunga na timu hiyo, katika msimu uliopita.

“Furaha kubwa ninaipata tangu nijiunge na Yanga, kiukweli sijutii maamuzi yangu niliyoyafanya ya kuichagua timu yangu hii ninayoichezea kwa moyo mmoja.

“Kwani nina amani kubwa hapa, nitaendelea kupambana nikiwa naichezea Yanga ili kuwapa furaha viongozi na mashabiki wetu kwa kuanzia msimu huu na huo mwingine unaokuja.

“Niwaahidi kuipa makombe tuliyoyabakisha katika msimu huu ambayo ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika ambako kote tumefuzu hatua ya Nusu Fainali,” alisema Aucho.

STORI NA WILBERT MOLANDI
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad