Kifupi unaweza kusema Yanga nzima ipo nchini Afrika Kusini baada ya kuwasili kwa mfadhili wao Ghalib Said Mohamed 'GSM' akiungana na viongozi wa juu wa klabu hiyo.
GSM amewasili leo akiungana na Rais wa Yanga, Hersi Said na makamu wake Arafat Haji ambao walitangulia na timu hiyo.
Viongozi wengine waliotangulia ni pamoja na wajumbe wa kamati ya Utendaji Munir Said, Alexander Ngai na Yanga Makaga ambaye aliwasili leo.
Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine na mjumbe wa kamati ya mashindano Mustapha Himba nao wapo hapa Afrika Kusini.
Mbali na viongozi hao wapo wadau wengine wa Yanga wameendelea kuwasili kuongeza hamasa kwenye Kambi yao.
Arafat, Himba, Munir, Ngai na Mtine ndio viongozi waliotangulia kwenye Kambi ya timu hiyo huku wengine wakibaki jijini Johannesburg wakitarajiwa kuwasili mjini Rustenburg kesho ambako ndiko timu hiyo imekita kambi yao.
Yanga itacheza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika Mei 17 mwaka huu dhidi ya wenyeji wao Marumo Gallants utakaoamua nani atinge fainali, huku Yanga wakiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.