Dodoma. Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa CCM, Abdalah Bulembo amesimulia jinsi Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alivyoagiza marehemu William Malecela maarufu ‘Lemutuz’ alipwe zaidi kutokana na blogu yake kukitangaza sana chama hiko.
Lemutuz ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela alifariki Mei, 14 mwaka huu jijini Dar es salaam katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na jana aliagwa nyumbani kwa Malecela Uzunguni jijini Dodoma.
Leo Jumatano Mei 17, 2023 Le Mutuz anazikwa katika kijiji cha Mvumi wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambapo viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza katika mazishi hayo.
Akizungumza katika mazishi hayo, Bulembo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa kuteuliwa amesema amemfahamu kwa muda mrefu marehemu Lemutuz na alimpokea jumuiya ya wazazi akitokea jumuiya ya Vijana (UVCCM).
Amesema kuna wakati walifanya ziara kuzunguka nchi nzima ya kukitangaza chama wakiwa pamoja na marehemu.
Bulembo amesema marehemu alitumia blogu yake ya Lemutuz kutangaza kile kilichokuwa kikifanyika katika mikutano hiyo hali ambayo ilimfanya Rais mstaafu Kikwete kupiga simu kwa Bulembo na kuagiza alipwe zaidi.
“Rais Mstaafu Kikwete akaniuliza wewe upo na William kila siku mnamlipa ? nikamwambia Mheshimiwa Mwenyekiti tunamlipa akasema sasa mlipeni sana, ninyi mnafanya kazi lakini ya William ni kubwa sana,”amesema Bulembo
Amesema Rais Msaafu huyo alisema Lemutuz alikuwa akikitangaza chama pamoja na kuongeza idadi ya wafuasi kipitia blogu yake.
Akimzungumzia Lemutuz amesema jamii imepoteza mtu makini ambaye alikuwa anaweza kuishi na mtu yoyote bila kujali rika.
Hata hivyo amewataka vijana wanaopata madaraka kuacha kupandisha mabega na kuacha dharau.
“Nataka kusema vijana mnaokuwa acheni kupandisha mabega, huijui kesho yako leo upo kesho haupo lakini wengine tukiwapa mikono mnatupa vidole,”amesema Bulembo.