Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini upungufu katika mfumo wa TTMS unaotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa miamala ya simu za mkononi ili kutoa uhakiki wa mapato.
Katika ripoti yake ya 2021/22 iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni, CAG Charles Kichere, amebaini tofauti kati ya viwango vya malipo vilivyopo kwenye kanuni na viwango vilivyotozwa kutokana na mfumo wa TTMS, kuchukua ada na kodi za miamala ya simu za mkononi kama zinavyotoka kwenye mifumo ya waendeshaji na kutokuwa na udhibiti wa kuthibitisha kuwa mifumo ya waendeshaji inatumia viwango sahihi.
CAG anasema katika Ripoti Kuu ya Ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) ya Mwaka 2021/22, upungufu huo unaweza kusababisha malipo ya kodi inayohitajika kuwa ya chini au ya juu.
Aidha, CAG anasema Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania, inahitajika kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa miamala ya simu za mkononi ili kutoa uhakiki wa mapato kwa kuzingatia Kifungu cha 4 - (2) (i) cha Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Tele-Traffic), 2021.
Kutokana na tofauti katika viwango vya malipo na kodi kwa miamala ya simu za mkononi, CAG anapendekeza TCRA iboreshe mfumo wa TTMS kuweza kukokotoa upya tozo ili kuhakikisha kuwa viwango sahihi vinatumika na kwamba ada na kodi zipo sahihi.
Kuhusu usuluhishi hahifu wa tozo za miamala ya simu za mkononi, CAG anasema ukaguzi ulibaini kuwa na utofauti kati ya kodi zilizoripotiwa katika mfumo wa TTMS wa TCRA na na kodi zilizowasilishwa kwa TRA na waendeshaji.
CAG anasema chanzo cha tofauti hizo kilichangiwa na utaratibu duni wa usuluhishi wa miamala, hivyo usahihi wa kodi za serikali hauwezi kuhakikishwa.
Katika eneo hilo, CAG anapendekeza TCRA iimarishe utaratibu wa usuluhishi kwa kuzingatia taarifa zilizoripotiwa kwa TRA na waendeshaji. Pia itekeleze usuluhishi baina ya mfumo wa TTMS na mfumo wa e-filing wa TRA kwa uthibitisho wenye ufanisi zaidi.
Kuhusu kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa miamala ya simu za mkononi isiyofanikiwa. CAG anasema amegundua kuwa ufuatiliaji wa miamala ya simu za mkononi isiyofanikiwa haufanywi katika mfumo wa TTMS.
CAG anasema alielezwa kuwa muundo wa TTMS haukuzingatia miama hiyo, sababu haipaswi kuwa na ada zaidi ya gharama za mtandao zinazohusiana na matumizi ya njia za USSD. CAG anapendekeza TCRA kuimarisha mfumo wa TTMS ili kujumuisha ufuatiliaji miamala isiyofanikiwa yaani Rollback Transactions.
Kadhalika, katika ripoti hiyo ya ukaguzi ya TEHAMA, CAG anasema ukaguzi wa mfumo wa TTMS katika Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano ya Tanzania (TCRA), uligundua tofauti katika viwango vya tozo kwa miamala ya simu, baina ya kiwango kilichotumika na kiwango kilichoanishwa kwenye kanuni, ambapo TTMS inachukua ada na ushuru wa miamala ya simu kutoka kwa mifumo ya waendeshaji bila kuhakiki ikiwa ni sahihi kulingana na kanuni.
Kwa kuongezea, CAG anasema amebaini usuluhishi usiotosheleza kwa ushuru wa miamala ya simu unapelekea kutofautiana kati ya ushuru ulioripotiwa katika TTMS na ushuru uliowasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) na waendeshaji.