ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania Sweden, Wilbroad Slaa, amesema haoni sababu inayowezesha wabunge 19 wanaoongozwa na Halima Mdee kuendelea kuwapo bungeni ilhali chama chao kilishafanya uamuzi dhidi yao.
Dk. Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alitoa kauli hiyo jana wakai wa mazungumzo maalum na Nipashe nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.
Alisema wabunge hao hawatakiwi kuwapo bungeni kwa kuwa hawana ridhaa ya CHADEMA na hakuna zuio la kisheria la kuwafanya kuendelea kuitwa wabunge wa viti maalum.
Mdee na wenzake walifungua shauri namba 36/2022 Mahakama Kuu Julai 22, 2022, wakiomba mahakama ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kisha itoe amri tatu.
Katika shauri hilo, wabunge hao wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama, iwalazimishe CHADEMA kuwapa haki ya kuwasikiliza na kuwekwa zuio kwa Spika wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua hatua yoyote hadi malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.
Katika mazungumzo na Nipashe, Dk. Slaa alisema anatambua uwezo wa baadhi ya wabunge hao, akiwatolea mfano Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko kwamba lishiriki kuwajenga. Ni kazi kubwa kujenga wengine wa mfano wa hao. Itachukua muda mrefu, lakini utaratibu uliotumika kuwaweka bungeni ni wa kibabe.
"Kwa muda mrefu nimekuwa ninakwepa kujibu hili swali kuhusu kina Halima Mdee. Sababu ya kutojibu ni kwamba mimi kichwani kwangu ninashindwa kuamini kwamba wale wanawake wameenda bila mtu fulani kupeleka majina. Kwa hiyo, nilikuwa ninatafuta. Pili, kwamba huenda walizungukana huko ndani (CHADEMA).
"Nikawa pia ninashindwa kumbana Spika kwa sababu kwa kawaida yeye anapelekewa majina na NEC. Kwa hiyo, nikategemea katika kipindi chote wanabishana atajitokeza mtu aseme kuna aliyeghushi, lakini hakuna aliyetokeza. Nikategemea atajitokeza wa kusema tume haikupeleka majina lakini hakuna aliyetokea.
"Nikategemea kuna atakayehoji Spika ndiye aliyekosea, lakini Spika ameendelea kulalamikiwa kuwa alipelekewa barua haraka baada ya uamuzi wa Baraza Kuu.
"Na wakati huo anapelekewa barua hapakuwa na zuio, nikafuatilia kesi mahakamani, hakuna yeyote anayehusika na haya niliyoyataja. Kesi iliyopo ni kuomba mahakama kwamba CHADEMA iwape fursa ya kuwasikiliza, hayo niliyoyataja yote hakuna hata moja lililopo mahakamani.
"Baada ya kuzingatia hilo, hoja inayokuja ni kwamba kama haya makubwa niliyoyataja hayakuhojiwa, tafsiri pekee iliyopo ni kwamba wakati CHADEMA ilipothibitisha uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwafukuza hapo katikati wakati huo hakuna chochote mahakamani na hapakuwa na pingamizi la Spika kuwaondoa. Kwa hiyo, ni kiburi tu cha Spika, hakutaka kuwaondoa.
"Spika ametafuta tu kisingizio watu wasioelewa wanaamini kwa kuwa kuna kesi iliyopo mahakamani, lakini wanashindwa kuunganisha ile kesi ni ya nini, ile kesi unataka tu wao kurudishiwa nafasi ya kwenda kusikilizwa. Sasa hiyo inahusiana nini na wao kuwapo bungeni?" alihoji Dk. Slaa.
KATIBA MPYA
Kuhusu hoja ya katiba mpya, Dk. Slaa alisema anaona hakuna nia ya dhati ya kupatikana katiba ya wananchi kwa kuwa hadi sasa hakuna hatua muhimu zilizochukuliwa ikiwamo kutengwa bajeti ya kuanzishwa mchakato huo.
"Tumeona kilichotokea mwaka 2019 na 2020, viongozi karibia wote hawajachaguliwa na wananchi. Sasa kwa sisi tunaojua nini maana ya uchaguzi, hiki kitu hatuwezi kukikubali.
"Ninajua kuna watu walisema kwani katiba inaleta chakula mezani? Huo ni upuuzi, ni fikra potofu, hakuna kitu duniani ambacho hakifanywi na katiba, nenda Marekani, Rais mstaafu ambaye sisi tunamlinda kwenye Katiba kule anashtakiwa.
"Nchi kama Marekani Rais hawezi kujiamulia tu kwa kuwa yeye ni Rais, hata Deni la Taifa kulipwa ni mpaka idhini ya Bunge. Juzi hapa Joe Biden akiwa katika Mkutano wa G7 wabunge wamemwambia imefika muda wa kulipa Deni la Taifa na tusipolipa tutaingia kwenye matatizo, amerudi haraka. Je, hapa Tanzania Kamati ya Bunge inaweza kumwita Rais kumwambia chochote?" Alihoji.
Dk. Slaa pia alizungumzia ubadhirifu wa mali ya umma uliotajwa katika ripoti mpya ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Alisisitiza haridhishwi na hatua zinazochukuliwa dhidi ya waliotajwa kuhusika na ubadhirifu huo.
Imeandikwa na Enock Charles na Zanura Mollel