Familia ya marehemu William Ernest aliyefariki jana katika Uwanja wa Mkapa alipokwenda kushuhudia mechi ya fainali ya kwanza ya Yanga dhidi ya USM Alger wanaomba msaada wa Serikali na Yanga ili kusafirisha mwili jijini Dodoma.
Akizungumza mtoto wa marehemu Dorrah William, amesema kwa sasa hali ya familia siyo nzuri hivyo wanaomba msaada ili wakampumzishe baba yao nyumbani kwao Mvumi Mission, Dodoma.
Amesema marehemu alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga na siyo mara yake ya kwanza kuhudhuria kwenye mechi za yanga pindi inapocheza akiwa na mashabiki wenzie kutoka Morogoro.
"Baba alikuwa anaipenda sana Yanga anaweza asifike nyumbani akaenda kuangalia mechi bila kuonana na sisi na hata mechi ya jana alikuwa amekuja akitokea Morogoro na aliondoka nyumbani asubuhi," alisema Dorrah.
Pia, amesema taarifa za msiba walizipata saa 1 usiku kutoka kwa Dk Kimaro akiwataka waende kumuona William kwani anaumwa na alipata majeraha sehemu ya kichwani kutokana na mkanyagano.
Naye shemeji wa marehemu Grace Lucas amesema wamepata pigo sababu marehemu ndiye tegemeo la familia na ana watoto wanaosoma.
"Mke hana kazi na hapa tulipo wamepanga hivyo hatuna chakula na mchana majirani walitusaidia ila jioni yetu hatuijui," amesema Grace.
Kuhusu klabu ya Yanga, Mwananchi limemtafuta meneja wa mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe ambaye amesema wameshawasiliana na familia kuona ni jinsi gani watakavyosaidia.
"Leo asubuhi tumekutana na ndugu wa marehemu katika Kituo cha Polisi Chang'ombe na tumewaambia kesho kama uongozi tutafika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa rambirambi," amesema Kamwe.
William alikuwa anajishughulisha na uuzaji wa nyama Morogoro na Dodoma na ameacha mke na watoto wanne ambao wawili ni wanasoma shule ya msingi.