Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kifo cha Bernard Membe kimemhuzunisha akisema mwanasiasa huyo, alikuwa zaidi kaka yake licha ya tofauti za kisasa zilizopo kati yao.
Membe ambaye ni waziri wa zamani wa Mambo ya Nje katika Serikali ya awamu ya nne amefariki dunia leo asubuhi Ijumaa Mei 12, 2023 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, Lema ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, amesema alifahamiana na Membe mwaka 2010, walipokutana bungeni tangu wakati huo walikuwa marafiki na familia zao zilikuwa na ukaribu.
“Huwa akija (Membe) Arusha tulikuwa tunakutana na kula chakula cha pamoja, vivyo hivyo nikiwa Dar es Salaam, nilikuwa nakwenda kwa Mama Membe ananipikia ugali. Nimesikitika kusikia habari, hata mke wangu (Neema), akisikia taarifa atahuzunika sana,”amesema Lema.
Lema ambaye ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, amesema walikuwa wanapishana na Membe katika kiitikadi na siasa, hasa masuala ya diaspora na misimamo ya Chadema kwa sababu mwanasiasa huyo alikuwa CCM, hata hivyo tofauti hizo hazikuwafanya kujenga uadui.
“Wakati alipopata misukosuko ya kisasa nilikuwa namfuatilia kwa karibuni, vivyo hivyo na mimi nilipopata changamoto alikuwa ananifuatilia. Membe alikuwa zaidi ya kaka familia yake imepoteza baba mzuri, Mama Membe amepoteza mume bora na mimi nimepoteza kaka na rafiki,”amesema Lema.
Mdogo wa mwanasiasa huyo, Tasilo Membe ameliambia Mwananchi kuwa saa 10 alfajiri kaka yake alianza kupata shida ya kifua ambako alikuwa akikohoa, ndipo saa 11 akakimbizwa Hospitali ya Kairuki kwa matibabu zaidi baada ya kuonekana akiishiwa nguvu.