Kaka wa Daktari Aliyeuawa Tarime Afunguka Kwa Uchungu "Nilikuwa njiani Kwenda Kumtembelea"


Anaandika Abdulkarim Malisa, kaka wa marehemu Dr.@isackathumansima.
________
Wiki iliyopita nilikua kikazi Kanda ya ziwa. Nilikujulisha ukaniambia nisiondoke bila kufika Tarime, nione unapofanya kazi, maana tangu upangwe huko sijawahi kufika.

Jumanne nikatoka Geita kwenda Chato. Jumatano nikaanza safari kutoka Chato kwenda Mwanza. Nikakupigia kuwa nitalala Mwanza ili alhamisi nimalizie safari. Ukapokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa.

Nikakutania upo mkoa wa Mara inabidi uwe imara. Nikakukumbusha enzi za shule ya msingi ukionewa unakuja kuniambia, naenda kuwapa "haki ya kikatiba" waliokuonea. Ulipoenda Ifunda Tech nilikushauri usimuonee mtu lakini jifunze kujitetea. Ukaniambia sasa hivi huonewi tena maana umeanza kupata kitambi. Wakati ule walikuonea maana hukua na mwili. Tukacheka na kuagana tukitarajia kuonana kesho yake.

Nikaingia Mwanza usiku. Nikakupigia simu hukupokea, nikakuandikia sms kuwa nimefika Mwanza na kesho nitakua Nyamongo, Tarime.

Alhamisi nikaamka saa 1 asubuhi. Nikakuta missed calls 32 kutoka kwa ndugu wa karibu. Kutokana na uchovu niliweka simu "silence" hivyo sikusikia wakati wanapiga. Lakini ilinishtua. Haikua kawaida kutafutwa mara nyingi hivyo.

Nikaona missed call ya mama na ndugu zetu wengine. Kabla sijawapigia nikasoma kwanza sms. Ooh my GOD. Nilijihisi nipo ndotoni. Eti umefariki? Nikasema haiwezekani, maana jana tumewasiliana na hata hii safari yangu naelekea kwako.

Mdogo wangu kwanini wamekufanyia ukatili huu? Uliwakosea nini? Mbona hujawahi kuwa na shida na mtu? Kwanini hawakusubiri hata nifike kwanza? Ningekutetea kama ilivyokua shule ya msingi. Singekubali kuina damu yako inamwagika mbele yangu, labda watuue wote. Ule usiku nilipokupigia simu hukupokea kumbe ulikua unapigania roho yako katikati ya mbwa mwitu wakali?

Safari yangu ya Tarime imeishia Mwanza. Badala ya wewe kunipokea Tarime, mimi ndio napokea mwili wako hapa Mwanza? Namuwaza mkeo na mwanao. Hawa walikuhitaji zaidi kuliko watu wengine. Lakini umewaacha mapema mno. Mkeo amebaki mjane kabla hata ndoa yenu haijafikisha mwaka mmoja. Mwanao amebaki yatima akiwa bado kachanga. Kwaheri mdogo wangu Isack. Mungu atatukutanisha tena. Moyo wangu unavuja damu 😭😭
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad