JESHI la Polisi mkoani Mwanza linatarajia kumfikisha mahakamani Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk. Hamis Kigwangalla kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mlinzi wake, Jumanne Omary (66).
Dk. Hamis Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kuchakata pamba kiitwacho Mwalujo Ginery kilichopo Kijiji cha Mwalujo wilayani Kwimba mkoani Mwanza, anatuhumiwa kutenda kosa hilo Mei 22 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, inaeleza kuwa hata mlinzi huyo atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo.
Kamanda Mutafungwa alisema Dk. Kigwangalla anatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi mguu wa kulia mlinzi wake huyo ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zinazodaiwa za uongo kwamba alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mbunge huyo.
Kamanda Mutafungwa alieleza kuwa katika kiwanda hicho kulitokea wizi wa mali mbalimbali za Sh. milioni 28.5, hali iliyozua mgogoro baina ya mmiliki wa kiwanda hicho na mlinzi wake.
Alidai kuwa Mei 22 mwaka huu saa 11 jioni, Dk. Kigwangalla alifika kiwandani kwake ambako kulitokea majibizano kati yake na mlinzi.
Alisema siku hiyo hiyo mlinzi huyo alitoa taarifa kituo cha polisi kuwa alishambuliwa na kupigwa risasi katika mguu wake wa kulia na kupatiwa PF3 na kwenda Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda huyo alisema kuwa Dk. Kigwangalla alihojiwa na polisi na kufunguliwa mashtaka ya kushambulia na sasa yuko nje kwa dhamana na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yake.
Vilevile, taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi ilieleza kuwa baada ya uchunguzi kufanyika, iligundulika kuwa mlinzi huyo hakuvunjwa mguu wala kujeruhiwa kwa silaha ya moto.
“Hivyo, mlinzi huyo naye anashikiliwa na kufunguliwa jalada la uchunguzi kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi na kuzua taharuki kwa jamii kuwa amepigwa risasi. Hivyo, naye anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yake,” alisema.
Kamanda Mutafungwa alieleza kuwa upelelezi wa kesi hizo mbili unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani huku uchunguzi wa tukio la wizi katika kiwanda hicho ambao uliripotiwa katika Kituo cha Polisi Kwimba unaendelea kufanyika na taarifa zaidi itatolewa pindi utakapokamilika.
Alisema Jeshi la Polisi linawataka wananchi mkoani humo kuchukua hatua sahihi za kisheria na kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokuwa na migogoro ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyombo vya dola au taasisi zenye mamlaka.
IPP