Kikwete: Membe alinitesa alivyohamia ACT-Wazalendo



Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema kuwa uamuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, kuhamia ACT-Wazalendo kutoka CCM mwaka 2020 na kuwania urais ulimpa wakati mgumu.


Amesema hajui kama ni Zitto Kabwe (Kiongozi wa ACT-Wazalendo) ndiye aliyemfuata Membe ajiunge na kukiimarisha chama chake au Membe ndiye aliyemfuata ili akuze demokrasia na aendeleze siasa.


Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 16, 2023 alipokuwa akitoa hotuba wakati wa misa ya kumuaga Membe aliyefariki Mei 12, 2023 katika hospitali ya Kairuki alikokuwa akipatiwa matibabu mpaka umauti ulipomkuta.


Amesema Membe alikuwa jasiri na hakuogopa jambo lolote pale anapoona haliendi sawa hivyo alipoamua kuhama chama ulikuwa uamuzi wake, ingawa yeye (Kikwete) ulimpa wakati mgumu.


Kikwete amesema hata hivyo uamuzi huo haukuathiri ujamaa wao kwa kuwa aliamini kwenye familia kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama anachokiona kinafaa.


"Ukweli uamuzi ule wa Membe ulinipa wakati mgumu wa kushirikiana naye lakini nashukuru baadae tulikuwa vizuri maana hasira zake ziliisha," amesema Kikwete.


Amesema hata hivyo anajua familia moja inaweza kuwa na wanachama wa Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, CCM lakini bado wanaendelea kushirikiana hivyo uamuzi wa Membe aliuchukulia wa aina hiyo.


Kikwete amesema hata hivyo mara kadhaa alifanya jitihada za kutatua changanoto zilizomfanya Membe aondoke CCM.


Bila ya kutaja kama alifanikiwa au la lakini kauli yake na kile kilichotokea mwaka jana baada ya Membe kurejea CCM kinaonyesha mafanikio ya jitihada zake.


Itakumbukwa kuwa Membe alikuwa akikosoa utawala wa Rais Magufuli kila mara hali iliyomfanya aonekane muasi na kuhojiwa na vikao mbalimbali vya chama na alivuliwa uanachama mwaka 2020.


Hata hivyo Membe aliendelea kuwa mkosoaji wa uendeshaji wa Serikali na chama uliokuwa chini ya Magufuli.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad