FISTON Mayele ndiye mchezaji wa Yanga ambaye anaonekana kumnyima usingizi kocha wa Marumo Gallants, Dylan Kerr ikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kupigwa kati ya timu hizo.
Yanga itaanzia nyumbani kwa Mkapa, Mei 10 mwaka huu kabla ya wiki moja baadae kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kumalizana na chama hilo la Kerr ambaye aliwahi kuzifundisha Simba na Gor Mahia kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kocha huyo raia wa Uingereza, hakuficha juu ya ubora wa Yanga na namna ambavyo mashambuliaji wake, Mayele amekuwa kwenye kiwango bora lakini alisisitiza kuwa hawapo kwenye hatua hiyo kwa bahati mbaya.
"Muda mwingine ni jambo zuri kujua mpinzani wako alivyo na ni wachezaji gani hatari ili kuwa na namna bora ya kukabiliana nao, ni miaka mingi kidogo tangu nifanye kazi Tanzania na Afrika Mashariki lakini bado moyo wangu upo huko, nimekuwa na marafiki ambao bado tunawasiliana,"
"Nitakuja kwa ajili ya Marumo na lengo letu ni kucheza fainali hivyo tutakuwa tayari kukabiliana na yeyote sio Mayele peke yake na timu nzima kwa ujumla ili tufanikishe mpango wetu," alisema Kerr.
Mayele ambaye anahofiwa na Kerr ameweka kambani mabao matano kwenye michuano hiyo sawa na Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants.
Kerr aliendelea kusema kuwa; "Unapokuwa nyumbani unatakiwa upate matokeo mazuri na ukiwa ugenini unatakiwa usikubali kufungwa, hii ni nusu fainali lolote linaweza kutokea, Yanga na naifuatilia Yanga, najua soka la Tanzania tangu nikiwa Simba."
Kerr alisema anaiona Yanga ikibadilika kiuchezaji tofauti na miaka miwili nyuma na ina wachezaji wazuri na sio kutoa mchezaji mmoja nyota tu kwenye timu.
"Ikiwa na mpira kutoka nyuma kwenda mbele inakuwa spidi tofauti na miaka miwili nyuma, wachezaji wote kwao ni wazuri."