Kocha wa zamani wa Yanga Mwinyi Zahera amesema timu yake ya zamani inanafasi ya kushinda dhidi ya USM Alger kama itajipanga vizuri kwa ajili ya mechi zao mbili za Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Zahera anasema Yanga ya sasa sio ile ya mwaka 2018 ambayo ilipoteza ugenini lakini ikafanikiwa kushinda nyumbani katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ukiingalia Yanga iliyocheza dhidi ya USM Alger mwaka 2018 na hii ambayo itacheza Fainali, kuna mabadiliko kwa 100%. Kila mmoja anajua historia ya Yanga wakati mimi nikiwa kocha.”
“Tulifungwa na USM Alger kwao [Algeria] lakini tuliwafunga kwenye mechi ya marudiano hapa [Dar].”
“Wakati tunapoteza kule Algeria kulikuwa na kundi kubwa la wachezaji waligoma kusafiri kwa sababu za madai ya mishahara [Chirwa, Ngoma, Yondani] hatukusafiri na mshambuliaji hata mmoja!
“Tulisafiri na jumla ya wachezaji 13 tu! Kwenye benchi tulikuwa na wachezaji wawili.”
Mwaka 2018 Yanga ilikuwa kundi moja na USM Alger [Kundi D] kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, katika mechi mbili dhidi ya USM Alger, Yanga ilipoteza 4-1 ugenini [Algeria] halafu ikashinda 2-1 nyumbani [Dar, Tanzania].