Korti yaruhusu DC kumpinga Rais Samia, kumstaafisha






Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu imemruhusu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini (DC), Komanya Kitwala kufungua shauri kupinga uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumlazimisha kustaafu bila kumpa sababu.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Lilian Mongela Mei 23, mwaka huu katika shauri la maombi lililofunguliwa na Kitwala dhidi ya Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Katika uamuzi huo, Jaji Mongela alimtaka Kitwala kufungua shauri hilo la mapitio ya mahakama la kupinga uamuzi huo wa Rais ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huo. Siku 14 zinaisha Juni 5.

Kitwala aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuhakiki mali za Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, aliteuliwa Julai 27, 2018 kuwa DC wa Tabora Mjini.


Kwa mujibu wa kiapo chake kilichounga mkono maombi hayo kabla ya uteuzi huo, alikuwa akifanya kazi PSSSF, akiwa Ofisa Sheria.

Hata hivyo, uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia Juni 19, 2021 na nafasi yake kujazwa na Dk Yahya Nawanda.

Baada ya uteuzi wake wa U-DC kutenguliwa alimwandikia barua Katibu Mkuu Utumishi, akiomba amrejeshe katika ajira yake ya awali PSSF.


Hata hivyo, barua yake hiyo haikujibiwa mapema, lakini baadaye alipokea barua ya Katibu Mkuu Kiongozi ya Agosti 15, 2022 iliyomfahamisha Rais amemstaafisha kwa maslahi ya umma.

Hakukubaliana na uamuzi huo ndipo akafungua maombi ya ruhusa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama ili kupinga uamuzi huo wa Rais.

Jaji Mongela katika uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kurejea sheria na uamuzi wa kesi mbalimbali za mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani, amekubaliana na hoja za wakili wa Kitwala, Jeremiah Mtobesya kwamba mwombaji amekidhi vigezo kustahiki kupewa ruhusa hiyo.

Alisema ni dhahiri mwombaji anaomba ruhusa kupinga uamuzi wa Rais unaomlazimisha kustaafu mapema, kwanza kwa kutumia kifungu cha sheria kisicho sahihi ambacho kinasababiaha usumbufu kwa mwombaji. Pia alisema jambo la pili linaloonekana katika kumbukumbu za shauri hilo ni kwamba hakupewa fursa ya kusikilizwa kabla ya kufikiwa kwa uamuzi na la tatu kwa kutokupewa sababu zote za uamuzi wa kumstaafisha kwa lazima.


"Kwa kuzingatia hoja zilizotolewa na mwombaji, zinazothibitisha kuwepo kesi ya kusikilizwa hususan kunyimwa haki ya kusikilizwa, ninaona kwamba maombi haya ni sahihi, yamekidhi matakwa ya kisheria kupewa ruhusa kufungua maombi hayo.

Katika shauri hilo, Kitwala alikuwa anaiomba mahakama imruhusu kufungua shauri la maombi ya Mapitio ya Mahakama, kupinga uamuzi wa Rais Samia wa Agosti 15, 2022 kumlazimisha kustaafu kabla ya muda wake kisheria.

Katika shauri hilo la mapitio atakalolifungua, Kitwala anataka kuiomba Mahakama hiyo iitishe na kisha kutengua na kutupilia mbali uamuzi huo wa Rais kwa kuwa amekwenda nje ya mamlaka yake kisheria dhidi ya kanuni ya haki asili na wa usumbufu kwake.

Pia anakusudia kuiomba mahakama hiyo imuamuru Katibu Mkuu, Utumishi amrejeshe katika ajira yake ya awali kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, kulipwa madeni ya mishahara yake na mafao mengine kuanzia Juni 28, 2021 mpaka tarehe ya kurejeshwa katika ajira yake.


Vilevile anakusudia kuiomba mahakama hiyo kuiamuru bodi hiyo ya wadhamini wa PSSSF kumrejesha katika nafasi yake ya awali.

Awali, Serikali ilijaribu kumzuia Kitwala kupata ruhusa hiyo baada ya kuwasilisha pingamizi la awal, ikiiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo la maombi ya ruhusa, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba.

Shauri hilo lilisikilizwa kwa njia ya maandishi na Kitwala aliwakilishwa na Wakili Mtobesya na wajibu maombi waliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Selina Kapange.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad