Kumekucha..Bungeni Wavurugana Mgomo Kariakoo, Spika aomba muda.

 


Sakata la mgomo ulioitishwa na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo, laibua mvutano kati ya Wabunge na Serikali huku Spika Dk Tulia Ackson; akiomba kupewa muda zaidi wa kujiridhisha na kinachoendelea sokoni hapo.


Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Dk Ashatu Kijaji leo Mei 15, 2023 amejikuta katika wakati mgumu Bungeni baada ya majibu yake kutowaridhisha watunga sheria hao, pale aliposema “Waliogoma Kariakoo ni kwa hiyari yao.”


Festo Sanga, Mbunge wa Makete (CCM) aliomba kutoa hoja ya kutaka Bunge lisitishe shughuli zake kwa muda ili lijadili kile alichosema kwamba “Kariakoo hali si nzuri” na kwamba Serikali inapoteza mapato kutokana na wafanyabiashara kufunga biashara zao.


Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wafanyabiashara wa soko hilo wamegoma kutokana na mgogoro wa matumizi ya mashine ya kielekroniki (EFD), Kamatakamata na alichosema masuala ya usajili.


Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema) ambaye alipinga majibu ya Waziri Dk Kijaji alisema kuwa shughuli zimesimama hadi Alhamisi na wafanyabiashara watakaofungua biashara zao wametahadharishwa kuwa watajuta na kitakachowakuta.


Hata hivyo Dk Kijaji aliendeleza msimamo wake kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na timu ya watu kutoka Wizara ya Fedha wanaendelea na mazungumzo kwa ajili ya jambo hilo.


Kutokana na mvutano huo, Spika Tulia ameomba muda wa kufuatilia jambo hilo na kwamba akijiridhisha ataruhusu lijadiliwe bungeni wakati wowote.


Hata hivyo Spika amesema kwa kauli ya Waziri na hoja za wabunge ni wazi kuwa ndani ya Kariakoo kuna tatizo ambalo lazima lifanyiwe kazi ili kupata ufumbuzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad