Simba imeondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Imeondoshwa kiume na mabingwa watetezi Wydad Casablanca kwa mikwaju ya penalti. Nani aliamini haya? Hakuna.
Baada ya Simba kupata ushindi mwembamba wa goli 1-0 kwa Mkapa, wengi waliamini kuwa atakwenda kupokea kipigo kizito pale Mohamed V Morocco, Uwanja unaotumiwa na Wydad. Nini kimetokea?
Simba imeruhusu goli moja pekee pale Morocco na kulazimisha mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Inashangaza sana. Simba waliwezaje? Subiri nitakwambia.
Wengine waliamini kuwa baada ya ushindi wa nyumbani, Simba wangekwenda kupaki basi pale Morocco. Waliamini Wachezaji wa Simba wangepoteza muda katika sehemu kubwa ya mchezo. Nini kilitokea? Simba hawakuwa na biashara hiyo. Walicheza mpira kwa dakika zote.
Licha ya Simba kuruhusu goli kipindi cha kwanza, walicheza vyema kwa muda wote uliosalia. Hadi kipindi cha kwanza kimemalizika Simba ilikuwa imepiga mashuti sita ambayo hayakulenga lango la mpinzani. Hii ni ishara tosha kuwa Walikuwa wakijaribu kushambulia.
Hawakuwa na papara sana wakiwa na mpira. Walikaba kwa nidhamu walipopoteza mpira. Walicheza kikubwa licha ya kuwa mpinzani wao ni bingwa mtetezi.
Walicheza kwa nidhamu kubwa. Hakukuwa na madhambi ya mara kwa mara. Ungeweza kufikiria mechi ngumu kama ile wachezaji kama Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Joash Onyango na wangetoka bila kuonyeshwa kadi ya njano? Ni ajabu na kweli.
Walicheza kwa adabu huku wakitekeleza majukumu yao. Hawakuwapa wapinzani nafasi ya kuwaonea sana. Hii ikasaidia Simba kucheza kwa uhuru zaidi. Ni wazi kuwa namna Simba walivyotolewa, watu wengi hawakuamini kama ingekuwa hivyo. Niliahidi nitakwambia wamewezaje.
Kwanza, niseme kwanza kuna sehemu tulimkosea heshima kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Amethibitisha kuwa ni kocha wa kweli.
Inaonekana kocha huyu alifanya kazi yake vyema kuwafahamu wapinzani vyema. Alifahamu Uzuri wao katika kuzuia na kushambulia.
Kabla Wydad hajakutana na Simba alikuwa amecheza mechi tano za hatua ya makundi bila kuruhusu goli. Walikuwa wa moto kweli. Lakini pamoja na uimara huo, Simba alipata goli dhidi yao pale kwa Mkapa.
Ni wazi kuwa Robertinho aliona namna ya kuvunja safu yao ya ulinzi na kuwaelekeza vijana wake cha kufanya. Ni bahati mbaya tu Simba ilipoteza nafasi nyingi katika mchezo ule. Ingeweza kupata ushindi mkubwa zaidi.
Ila pale Morocco walicheza kibabe. Waliwakabia wapinzani wao kwenye eneo lao. Walirudi haraka kukaba walipopoteza mpira. Walikaba nafasi zaidi kuliko mtu.
Hawakuwapa Wydad nafasi kubwa ya kufurahia mpira na kuanzisha mipango. Hii ndio Simba ya Robertinho.
Imeimarika sana. Inacheza soka safi na mipango. Ni hatari pia inapokushambulia. Kocha huyu Mbrazili ndio amefanya tuanze kumheshimu Kibu Denis tena.
Amebadilisha aina yake ya uchezaji. Kibu mbali na uwezo wake mkubwa wa kusaidia kukaba, anashambulia vizuri sasa. Hana maamuzi mengi ya papara kama zamani. Maisha yamebadilika chini ya Robertinho.
Kocha huyu ni mkali wa mbinu na uthubutu. Nani aliamini kuwa Ally Salim angecheza mechi zote mbili dhidi ya Wydad na akaruhusu goli moja tu?
Wengi waliwaza kuwa atafungwa mengi. Nini kimetokea? Amekuwa katika kiwango bora sana. Ni busara za kocha wake Robertinho: