Geita. Watu wanaosadikika kuwa ni majambazi wamevamia na kupora fedha kwenye maduka 14 yanayotoa huduma za kifedha katika eneo la Njiapanda ya Kanyala Mji mdogo wa Katoro Mkoa wa Geita.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Cornel Magembe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Mei 23 na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwabaini waliohusika.
Amesema hadi sasa hasara kamili haijafahamika na kusema tukio hilo halikubaliki na kuwataka wannachi kushirikiana na serikali kuimarisha ulinzi na kuhakikisha wanalinda mali zao na za wengine.
“Kama serikali tunaendelea kutimiza wajibu wetu kupitia jeshi la polisi kuhakikisha tunalinda mali na raia kwa pamoja,” amesema Magembe.
Wakizungumza kwenye eneo la tukio baadhi ya wananchi ambao maduka yao yameporwa wamesema eneo hilo linalindwa na walinzi saba wa kampuni ya ulinzi na kushangazwa watu kuvamia maduka 14 kwa wakati mmoja bila walinzi hao kugundua.
Katibu wa eneo la soko hilo, Jonathan Stanslaus amesema alipata taarifa kutoka wasamaria wema usiku na kuelezwa kuna watu wamevamia maduka na alitoa taarifa polisi na walipofika wamekuta kofuli zimevunjwa na maduka hayo kuporwa fedha na simu.
“Nilipigiwa simu na mwanachi saa 7:30 usiku akidai eneo la maduka kuna watu wamevamia niliwasiliana na polisi na baada ya muda tulifika hapa tumekuta wamevunja kufuli zipo zilizopigwa kwa nyundo na nyingine wamekata kwa msumeno,” amesema.
Hata hivyto amesema hadi wakati huo, walinzi hawakuwepo katika eneo lao la kazi na walirudi baada ya saa moja.
“Hawakupiga filimbi wala kutoa ishara yoyote ili majirani waamke. Tukio hili linaumiza sana ukiangalia na hali ya maisha ilivyo,” amesema Marco Chuma ambaye ni mmoja wa wenye maduka hayo.
Jonas Chupa anayeishi karibu na maduka hayo amesema usiku alisikia kelele na za watu wakigonga mlango na kwamba tukio hilo la uvamizi lilitumia zaidi ya dakika 40 na baada ya kumaliza kundi hilo la watu lilipita pembeni ya nyumba yake na kuondoka.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ludete, Martine Matiba amesema maduka 14 yanayotoa huduma za kifedha za simu na zile za benki yalivamiwa na kuporwa na kwamba hadi sasa bado haijafahamika kiasi cha fedha kilichoporwa na kwamba wanaendelea kuorodhesha na taarifa kamili watazitoa baadae.
Juhudi za kupata taarifa kutoka Jeshi la polisi mkoa wa Geita hazikuzaa matunda baada ya kufika ofisini kwa kiongozi huyo na kupewa taarifa kuwa yuko kwenye kikao.
Hili ni tukio la pili kutokea Wilayani Geita ambapo Aprili 23, 2023 kundi la watu 10 wanaosadikiwa kuwa wezi walivamia na kupora maduka nane ya huduma za kifedha yaliyopo kata ya Nyawilimwilwa Wilaya ya Geita na kuiba kiasi cha Sh 31.2 milioni na kisha kuwajeruhi walinzi saba waliokuwa wakilinda maduka hayo.