Kamati ya mashindano ya Chama cha soka Nchini Uhispania (RFEF) imetoa maamuzi juu ya sakata la winga wa Real Madrid, Vini Jr ambapo imefuta kadi nyekundu aliyopewa Mbrazil huyo kwenye mchezo wa kipigo cha 1-0 cha Real Madrid dhidi ya Valencia.
RFEF imefikia uamuzi huo kwa kuwa adhabu hiyo ilitolewa chini ya ushahidi batili. Mwamuzi wa VAR hakumwekea Mwamuzi wa Kati picha zote zinazohusu matukio yaliyopelekea adhabu hiyo kutolewa.
Aidha Kamati hiyo imethibitisha kuwa klabu ya Valencia imetozwa faini ya Euro 45,000 pamoja na kuufungia kwa mechi 5 upande wa uwanja wa Mestalla uitwao Mario Kempes kusini, ambapo vitendo vya ubaguzi wa rangi kwa Vini Jr vilitokea.
Vinicius Jr atakuwa huru kuitumikia klabu yake hiyo leo Real Madrid itakapomenyana na Rayo Vallecano majira ya saa 2:30 usiku katika dimba la Santiago Bernabeu.