Tabora. Utata umeendelea kutawala tukio la pacha waliozaliwa na kufa, kisha viungo vyao kunyofolewa macho, kukatwa ulimi na kuchunwa ngozi kwenye paji la uso katika kituo cha afya Kaliua, kufuatia kukwama kwa uchunguzi kwa kile kilichodaiwa baba kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili wakamilishe kazi hiyo.
Tukio hilo lililogusa hisia za wengi linadaiwa kutokea Mei 9, mwaka huu, Musaneza Benson (25) alijifungua pacha waliofariki muda mfupi baada ya kuzaliwa na siku iliyofuata maiti zilikutwa zikiwa zimeondolewa baadhi ya viungo.
Juzi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hatua zimeanza kuchukuliwa na kumwagiza Mganga Mkuu Mkoa wa Tabora kusimamia vema weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya.
Jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alilieleza Mwananchi kuwa uchunguzi umekwama kutokana na baba mzazi wa watoto hao, Issa Raphael kutokapatikana ili kushuhudia uchunguzi huo unavyofanyika kwa kuwa ni muhimu.
Hata hivyo, Raphael, aliyezungumza na Mwananchi jana alipinga madai hayo akisema hakuna aliyemfuata kuhusu suala hilo.
Alieleza kuwa Mei 15, 2023 alikwenda Urambo kwa ajili ya uchunguzi wa miili ya watoto wake na alitoa nauli ya watu saba, akiwemo na mkewe.
"Niligharamia nauli za watu saba kwenda kuungana nami kwa ajili ya uchunguzi ambao haukufanyika. Tulifika Hospitali ya Wilaya ya Urambo saa 6:30 mchana tukiwa na askari wa upelelezi mmoja, tulisubiri hadi saa 1:30 usiku hakuna kilichofanyika tukaondoka.
"Dakika 40 baada ya kuondoka wakanipigia simu turudi, muda wote huo tuliowasubiri ndio wanasubiri usiku, nami nikawaambia kwamba nimetumia gharama zangu na wao kuniambia kesho yake niende watanigharamia wakakubali. “Siku iliyofuata mke wangu alikuwa anaumwa, nikashindwa kwenda, tangu hapo hawajanitafuta tena," alisema.
Tukio lilivyokuwa
Mei 9 mwaka huu, Raphael alimpeleka kituo hicho cha afya mkewe akiwa katika hatua za mwisho za kujifungua na alifanikiwa kupata watoto pacha.
Alisema kwa kuwa Kituo cha Afya Kaliua hakina uwezo wa kuhudumia watoto njiti, waliwapa rufaa kwenda hospitali teule ya wilaya yenye mashine za kuhudumia na kwa kuwa kituo hakina gari la wagonjwa, waliambiwa wakatafute usafiri.
“Nikamuacha mke wangu na watoto wakiwa wazima wa afya, nikaenda kutafuta usafiri. Muda huo haikuwa rahisi kupata gari, nikapata bajaji. Tulipofika wahudumu wakasema tusubiri wawaandae watoto,” alieleza.
Alisema wahudumu wakasema waendelee kusubiri na ilipofika saa sita, dereva wa bajaji akataka kuondoka na alipowauliza kwa mara nyingine walimweleza kuwa wanamalizia kuwaandaa watoto.
Baba huyo alisema alimwambia dereva angemuongezea malipo, hivyo asubiri kidogo na baadaye wahudumu wakatoka na kuwaambia bahati mbaya watoto wamefariki, hivyo wakawaahidi kuwapatia miili yao kesho yake asubuhi.
"Baada ya wazazi kujulishwa kuhusu vifo vya watoto hao na kwa vile ilikuwa ni usiku, tuliamua kuiacha miili hadi siku iliyofuata na dada yangu aitwaye Lucia Lucas alikwenda kukabidhiwa miili hiyo kwa ajili ya maziko.
"Wakati wanaandaa miili hiyo kwa ajili ya maziko, aligundua mtoto mmoja ameondolewa ngozi kwenye paji la uso wake pamoja na kuharibiwa jicho moja la upande wa kulia," alisema Raphael.
Mwananchi