Mhadhiri Msaidizi wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Maria Erasmus ametoa tahadhari za kiuchumi endapo maeneo ya starehe yataendelea kufungwa kutokana na changamoto za ukiukwaji wa agizo la kudhibiti kelele zinazozidi viwango husika.
Maria amesema kufungia maeneo ya starehe 89, Serikali itapoteza mapato mengi kupitia mnyororo unaohusisha biashara hizo ikiwamo kodi ya Serikali kila eneo la starehe, mapato ya mfanyabiashara pamoja na kampuni husika za uzalishaji kupunguza mapato.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Mei 10, 2023 wakati wa mjadala wa TwitterSpace ya Mwananchi yenye mada ya kufungia baa, kumbi za starehe kwa sababu ya kelele ni suluhisho ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Mjadala huo unaakisi uamuzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufungia jumla ya baa na kumbi za starehe 89 baada ya kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango husika.
“Pia wasafirishaji, wauza chakula maeneo hayo watapoteza mapato maeneo hayo, ingawa sio ajira rasimi wanajipatia kipato, kila baa ikiwa na wafanyakazi watatu kwa hizo 89 ni ajira nyingi, kufungulia baa 20 kati ya 89 bado kuna wengine wanaendelea kuathirika.” amesema
Mhadhiri huyo amesema,“ninaamini hata wakulima huko vijiji wakakutwa na athari hizo, wakulima wa ndizi zinazouzwa kwenye baa hizo, mfano nauza mikungu kumi ila sasa nauza mitano, tayari ni hasara.”
“Pia, mabenki, waliokopa watashindwa kulipa na benki zitapunguza uwezo wa kukopesha wengine zaidi, hata sekta nyingine zitaathirika kwa namna hiyo.”
Akishauri, Maria amesema,“NEMC wangefanya semina elekezi, inawezekana wanajua sheria na katazo hilo la kelele lakini kwa kupuuza , wamechukulia mazoea, walitakiwa kupatiwa majadiliano mara kadhaa, semina na kuelimisha faida na athari za kelele hizo, namna gani wafanye.
“Pia, Serikali ingetenga maeneo maalumu ya sehemu za starehe hizo, kuhamisha wafanyabiashara maeneo ya makazi kuhama kwa muda na kubuni teknolojia itakayothibiti kelele, ikiwezekana kifaa cha kupiga kelele endapo muziki utaongezeka kwa kiwango fulani, “ameshauri Maria.
“Lakini pia tujifunze kwa wenzetu nje wamefanikiwa kwa namna gani na kuongeza faini pia ili watu waweze kutii sheria.”
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka akichangia kwenye mjadala huo amesema, wahusika wanapaswa kuzingatia sheria na kanuni ili kutowaathiri wengine kwa kelele.
Amesema hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa wale wote watakaoendelea kukiuka taratibu na kusisitiza sheria zilizopitishwa na Bunge zinapaswa kuheshimiwa na wale wote wasioridhika na uamuzi unaochukuliwa wanaweza kukata rufaa kwa waziri ama kwenda mahakamani.