WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka wazi rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mitaala toleo la 2023, ikiwataka wadau kutoa maoni.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Katika rasimu hizo, umri wa kuanza darasa la kwanza umepunguzwa, muda wa elimu ya lazima umeongezeka huku masomo mapya ya lugha, Tehama na stadi za maisha yakizingatiwa ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
Mapendekezo ya rasimu hizo yalitolewa jana na wizara hiyo kwa umma kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Inapendekezwa kuwa kwenye sera hiyo umri wa kuanza darasa la kwanza umepunguzwa kutoka miaka saba hadi sita, kama ilivyo katika nchi nyingi duniani huku muundo uliorekebishwa ukiruhusu mwanafunzi kukamilisha mzunguko wa masomo kwa muda mfupi zaidi.
Muundo katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo utakuwa 1+6+4+2/3+3+, kwa maana ya mwaka mmoja wa elimu ya awali, miaka sita ya elimu ya msingi, miaka minne ya elimu ya sekondari ngazi ya chini, miaka miwili ya elimu ya sekondari ngazi ya juu au miaka mitatu ya amali sanifu na miaka isiyopungua mitatu ya elimu ya juu.
Vilevile, elimu ya lazima itajumuisha elimu ya msingi na elimu ya sekondari ngazi ya chini na itatolewa kwa miaka 10. Lakini kila mtoto mwenye umri wa miaka sita na ambaye amepata au hakupata elimu ya awali kwa mujibu wa sheria, apatiwe elimu ya lazima itakayotolewa kwa muda wa miaka 10 ili kumwezesha mwanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, kuwa na ufahamu wa jumla na pia kupata umahiri ikiwamo maarifa na ujuzi kulingana na matakwa ya ngazi hiyo.
Pia, elimu ya awali itakuwa ya mwaka mmoja kwa watoto wenye umri wa miaka mitano kwa kuzingatia mahitaji yao, mazingira na hali halisi ya upatikanaji wa rasilimali nchini.
Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa muda wa kukamilisha elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali unalenga mwanafunzi kupata ujuzi na maarifa stahiki kwa kuzingatia mfumo wa tuzo wa taifa huku elimu ya msingi na sekondari katika mfumo wa umma ikitolewa bila ada.
Kadhalika, sera hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza ushiriki wa wasichana katika elimu ya amali na elimu ya juu hususan katika fani za sayansi, Hisabati na teknolojia.
Kuhusu matumizi ya lugha, serikali itahakikisha kuwa lugha za Kiswahili, Kiingereza na nyingine za kigeni zinafundishwa kwa ufasaha na ufanisi, lugha ya alama ya Tanzania na maandishi ya Breli zitatumika ngazi zote za elimu na mafunzo.
LUGHA YA KUFUNDISHIA
Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia katika elimu ya awali na elimu ya msingi, isipokuwa masomo ya lugha za kigeni na katika shule zitakazoomba kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia.
Lugha ya Kiingereza itatumika kufundishia kuanzia ngazi ya sekondari ya chini, isipokuwa somo la Kiswahili, masomo ya lugha za kigeni na katika shule za sekondari na vyuo vitakavyoruhusiwa kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia.
Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia somo la Historia ya Tanzania na Maadili ili kujenga na kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
YALIYOMO
Maeneo ya ujifunzaji yamejikita katika utamaduni, elimu ya imani, sanaa na michezo, lugha ya mawasiliano, rejea maeneo ya ujifunzaji, stadi za awali za maisha, afya na mazingira.
Mapendelezo ya mitaala kwa darasa la kwanza na la pili, masomo ni kusoma, kuandika, Demonstrate Mastery of Basic English Language Skills, Hesabu, kuthamini utamaduni, sanaa na michezo, kutunza afya na mazingira.
Masomo kwa darasa la tatu hadi la sita ni Kiswahili, English, Kifaransa, Kichina, Kiarabu, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili, Elimu ya Dini, Sanaa na Michezo, Sayansi na Jiografia na Mazingira.
Kwa elimu ya sekondari hatua ya chini masomo ni Historia ya Tanzania na Maadili, Historia, Jiografia, English, Literature in English, Kiswahili, Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Michezo, Baiolojia, Kemia, Fizikia, Kilimo, Hisabati, Additional Mathematics, Sayansi ya Kompyuta na Utunzaji wa Taarifa za Fedha (Book Keeping).
Pia masomo ya Elimu ya Biashara (Business Studies), Ushoni (Textiles and Garment Construction), Sanaa Sanifu (Fine Art), Muziki (Music), Sanaa za Maonesho (Theatre Arts), Maarifa ya Nyumbani (Home Management), Chakula na Lishe (Food and Nutrition), Elimu ya Dini ya Kikristo (Bible Knowledge), Elimu ya Dini ya Kiislamu na Fasihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa umahiri mkuu na umahiri mahususi, elimu ya sekondari hatua ya juu ni Historia, Jiografia, Elimu ya Dini ya Kikristo (Divinity), Elimu ya Dini ya Kiislamu, Kiswahili, English, Kiarabu, Kifaransa, Kichina, Fizikia, Kemia, Baiolojia, Chakula na Lishe, Sayansi ya Kompyuta, Hisabati, Hisabati Tumizi (Basic Applied Mathematics).
Pia masomo ya Kilimo, Historia ya Tanzania na Maadili, Michezo, Sanaa Sanifu, Muziki, Sanaa za Maonesho, Ushoni, Mawasiliano ya Kitaaluma, Elimu ya Biashara, Uhasibu, Uchumi, Fasihi ya Kiswahili na Literature in English.
Kwa upande wa masomo, umahiri mkuu na umahiri mahususi-Stashahada ya Ualimu na Stashahada ya Ualimu (Elimu Maalum), Elimu ya Awali na Astashahada ya Elimu ya Ukufunzi wa Karakana/Maabara ni Misingi ya Kinadharia, Mbinu za Ufundishaji, Ualimu kwa Vitendo, Masomo ya Jumla, Lugha na Mawasiliano.
Akizungumza na waandishi jijini hapa, Prof. Mkenda alisema serikali imeamua kutoa rasimu hizo ili kupata maoni na mwisho wa kuyapokewa ni Mei 31, 2023. Baada ya hapo rasimu hizo zitapelekwa katika ngazi za uamuzi mwezi ujao.
Waziri Mkenda alisema kuwa leo wizara itafanya semina kwa wabunge kuwapitisha katika rasimu hizo na Mei 12 hadi 14 kutafanyika kongamano kubwa la kitaifa jijini Dodoma la kuzijadili.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, alisema kongamano hilo ni la kimataifa na wamewashirikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kutoa maoni yao na uzoefu wao katika nchi wanazoishi.