Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Samuel Gwamaka amesema jumla ya baa na kumbi za starehe 89 zimefungiwa baada ya kubaini kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango vinavyotakiwa.
Dk Gwamaka amesema baa na kumbi hizo za starehe zimebainika katika operesheni iliyofanyika ndani ya wiki moja katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.
Ameeleza hayo leo Jumatatu, Mei 8, 2023 wakati akitoa mrejesho wa msako walioufanya kati ya NEMC na jeshi la polisi kubaini baa na kumbi za starehe zinazopiga muziki kwa sauti ya juu ambayo ni kinyume cha sheria ya mazingira ya mwaka 2014.
"Tumebaini na kufunga baa na kumbi za starehe 19 za Kinondoni, 25 Ilala, Kigamboni 22 na Temeke 12, jijini Dodoma ni tano na Mwanza ni sita. Maeneo haya tulioyafunga ni sugu na haikuwa mara kwanza kuwaonya hawa tuliowafungia,” amesema
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira ( NEMC), Dk Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya kubaini baa na kumbi za starehe zinazopiga kelele zilizidi kiwango.
Huku akiongeza kusema, "Huko nyuma tulishawaonya na kuwaadhibu kwa kuwapiga faini, lakini waliendelea kukaidi, miongoni baa sugu ni Bodroom, Wavuvi Camp, Wherehouse, Avoco, Kitambaa Cheupe.Wengine ni Element, Chako ni Chako, Rainbow Gentlemen, Liquid na Soweto."
Kwa mujibu wa bosi huyo wa NEMC, wamefikia uamuzi wa kuwafungia kwa sababu sio mara kwanza kwa baa na kumbi hizo kufanya makosa hayo, licha ya NEMC kuwaonya kwa nyakati tofauti.
Amesema baada ya kuwafungia baadhi ya wamiliki wa baa na kumbi wamefika ofisi za NEMC kuomba msamaha.