Panga Zito Lapita na Wachezaji Tisa Simba Kuingiza Majembe Mapya




Kikosi cha Simba.
SIMBA hawataki utani, haraka wamepanga kuchukua maamuzi magumu ya kuachana na wachezaji tisa kuelekea msimu ujao, huku wakiingiza majembe mapya.

Timu hiyo, imefikia uamuzi huo baada ya juzi Jumapili kufungwa mabao 2-1 na Azam ambayo yameifanya kuondolewa katika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, mchezo uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Ikumbukwe kuwa, Simba iliweka nguvu zao katika michuano hiyo baada ya kutokuwa na nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Msimu huu, Simba imekosa makombe matano iliyoshindania ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Kombe la Mapinduzi na Ligi ya Mabingwa Afrika.


Wachezaji baadhi wanaotajwa kuwepo katika mipango ya kusajiliwa na Simba msimu ujao ni beki wa kati wa Rayon Sports ya Rwanda, Abdul Rwatubyaye, kiungo wa Geita Gold, Edmund John na kipa wa Vipers FC, Alfred Mudekereza.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, haraka mabosi wa Simba wamefikia makubaliano ya kuachana na wachezaji tisa ambao ni Joash Onyango, Nassoro Kapama, Habib Kyombo.

Wengine ni Mohammed Ouattara, Jimmyson Mwanuke, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Ismail Sawadogo na Victor Akpan, huku wengine wakijadiliwa akiwemo Erasto Nyoni na Peter Banda.

Alisema kati ya wachezaji ambao watakutana na panga hilo, kati yao mikataba inamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku wengine wakiivunja.

“Hakuna jinsi ni lazima tuachane na baadhi ya wachezaji ili tupate nafasi ya kuisajili wengine watakaokiimarisha kikosi chetu msimu ujao.

“Tayari yapo baadhi ya majina yaliyokabidhiwa kwa uongozi kutoka kwa kocha wetu Robertinho (Roberto Oliveira), kati ya hao tutakaoachana nao wapo wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu na wengine tunaivunja,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Lipo wazi, ni lazima baadhi ya wachezaji tuwape mkono wa kwa heri kwa maana ya kuachana nao mwishoni mwa msimu huu.


“Uongozi utakutana kumfanyia tathimini mchezaji mmoja mmoja kwa kuangalia kiwango chake na msaada wake katika timu ambao ameutoa msimu huu, tunataka kuwa na wachezaji wapya watakaotuvusha Nusu Fainali ya michuano ya Afrika, tumechoka kila msimu tunaishia Robo Fainali.”

STORI NA WILBERT MOLANDI
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad