RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza kurejesha mpango wa nyongeza ya mishahara kila bila kutaja viwango ili kudhibiti mfumuko wa bei. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, leo tarehe 1 Mei 2023 mkoani Morogoro, Rais Samia amesema nyongeza hiyo ya mishahara itaendelea kila mwaka, baada ya zoezi hilo kusitishwa kwa muda.
“Kuna nyongeza za mishahara za kila mwaka ambazo zilisitishwa kwa muda, nikaona mwaka huu nizirudishe, nyongeza hizo za kila mwaka zitaanza mwaka huu na zitaendelea kila mwaka,”
“Ndugu zangu wafanyakazi kile watu walichozoea tukiseme hapa ili wapandishe bei madukani mara hii hakuna tunakwenda kufanya mambo polepole, wasione tumeongezeana kitu gani ili mwenendo wetu wa bei uwe salama,” amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali yake itaendelea kupandisha vyeo na madaraja ya watumishi wa umma.
Aidha, Rais Samia amewataka watumishi wa umma kufanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi ili Serikali iweze pata fedha za kuwalipa mishahara na stahiki nyingine.