MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Namungo na Simba umemalizika kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi kwa timu hizo kufungana bao 1-1.
Katika mchezo huu Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa mshambuliaji wake, Jean Baleke kabla ya Hassan Kabunda kuisawazishia Namungo dakika ya 39 kufuatia kipa, Ally Salumu kuutema mpira ndani ya boksi.
Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 16 mwaka jana, Namungo ilifungwa bao 1-0 lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Moses Phiri dakika ya 32.
Katika mchezo wa leo licha ya timu hizi kuonekana kuleta ushindani pindi zinapokutana ila rekodi zinaonyesha Namungo ni wanyonge kwa Simba kwani tangu ipande rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 haijawahi kushinda.
Tangu msimu huo timu hizi zimekutana mara nane ambapo Simba imeshinda michezo mitano huku mitatu ikimalizika kwa sare ambapo kati ya hiyo imekubali nyavu zake kutikiswa jumla ya mabao 15 huku wao wakifunga sita tu.
Mchezo huu ambao umepigwa Mei 3 unarudisha tena kumbukumbu ya mechi baina ya timu hizi uliochezwa pia Mei 3, mwaka jana wakati miamba hii ilipokutana kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi na kutoka sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo huo mabao ya wenyeji Namungo yalifungwa na Jacob Masawe anayeendelea kuwepo kikosini na Obrey Chirwa aliyepo Ihefu huku yale ya Simba yakifungwa na Shomari Kapombe pamoja na Kibu Denis ambao bado wapo.
Katika mchezo wa leo mwamuzi wa kati atakuwa ni Ester Adalbert kutoka Singida akisaidiwa na mwamuzi namba moja, Anold Bugado (Pwani) na Credo Mbuya (Mbeya) huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Abdallah Lisakasa wa Lindi.
Huu ni mchezo wa pili kwa mwamuzi, Ester Adalbert kutoka Singida kuichezesha Simba msimu huu kwani mara ya kwanza ni dhidi ya Mbeya City Januari 18, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa na kikosi hicho cha Robertinho kikashinda 3-2.
Bao la Baleke linamfanya nyota huyo kufikisha mabao manane ya Ligi Kuu Bara ndani ya timu hiyo tangu aanze kuichezea Januari mwaka huu akitokea Nejmeh ya Lebannon aliyokuwa akiichezea kwa mkopo akitokea TP Mazembe.
Kocha wa Simba Roberto Oliveira 'Robertinho' huu unakuwa ni mchezo wa nane kwake kuiongoza timu hiyo katika Ligi Kuu Bara tangu alipoteuliwa Januari 3, mwaka huu ambapo kati ya hiyo ameshinda sita na kutoka sare miwili tu.
Sare ya kwanza kwa Robertinho ilikuwa ni ya 1-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 21, mwaka huu.
Katika michezo hiyo safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga jumla ya mabao 16 huku eneo la ulinzi likiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano tu.
Katika michezo 27 ambayo Namungo imecheza imeshinda 10, sare sita na kupoteza 11 ikiwa nafasi ya sita na pointi 36.
Kwa upande wa Simba katika michezo 27 imeshinda 19, sare saba na kupoteza mmoja tu ikishika nafasi ya pili na pointi 64.