Imetimia miaka 25 tangu ajali ya basi iliyosababisha vifo vya abiria 96 na majeruhi 9, ilipotokea jioni ya tar 3/5/1998. Kihistoria haijawahi kutokea ajali mbaya ya basi iliyoua watu wengi kama hiyo.
Mimi ni miongoni mwa wale 9 tulionusurika kwa neema ya Mungu. Ajali hii ilihusisha basi la kampuni ya NO CHALLENGE ambayo baada ya ajali ilibadili jina na kujiita TASHRIF. Ajali ilitokea Mkoani Tanga, Wilaya Muheza, kijiji cha Kibanda. Bus lenye namba za Usajili TZK 960 lilikuwa likitoka Tanga kuelekea DSM.
Kipindi hicho kulikuwa na mvua nyingi zilizobatizwa jina Mvua za El-Nino. Tulipofika kijijini hapo tulikuta mabasi mengi yamesimama kutokana na kujaa maji kwenye mto. Kuanzia mabasi makubwa hadi madogo kama Coaster, Hiace na gari binafsi.
Kijiji cha Kibanda kuna mto uitwao Msangazi. Ulikua umejaa maji. Basi letu lilijaribu kuvuka ng’ambo ya pili ili kuendelea na safari. Baadhi ya abiria wa mabasi mengine walidandia basi letu ili wavuke kuendelea na ratiba zao. Lakini halikuweza kufika ng’ambo. Lilisombwa na maji. Likasukumwa mtoni na kuzama kabisa.
Watu 96 wakapoteza maisha, wakiwemo wale waliodandia. Sehemu kubwa ya abiria walifia ndani ya basi kwa kushindwa kutoka. Wachache waliotokea madirishani walikufa kwa kusombwa na maji yenye kasi ya mto huo. Ilikua simanzi kubwa.
Pamejengwa mnara wa kumbukumbu ya wafu na majina yao. Lakini naambiwa vijana wa vyuma chakavu wamekwanyua kibao kilichokuwa kimeorodhesha majina ya wafu 72 waliotambulika na wengine 24 ambao hawakutambuliwa.
Moja ya ajali za barabarani ambapo Basi lililotumbukia kwenye Mto Enziu katika Kaunti ya Kitui nchini Kenya, Desemba 5, 2021. (Picha ya Fred Mutune/Xinhua).
Katika wale 9 tuliosalimika, alikuwepo Mzee Ramadhani Kimbunga Dereva wa basi hilo. Bahati mbaya pamoja na kuokoka kwenye ajali hiyo alikuja kufa miezi michache baadae kwa kifo cha kawaida. Manusura wengine wawili nao walishafariki kwa nyakati tofauti, na tuliosalia hai mpaka sasa ni 6 tu.
Baada ya ajali hiyo kampuni ya NO CHALLENGE ikabadili jina kuwa TASHRIF. Ikumbukwe kabla ya hapo ilikua ikiitwa AIR SHENGENA. Ilipopata ajali ya kugonga treni Korogwe mwaka 1996 ikaitwa NO CHALLENGE. Na baada ya ajali ya maji Muheza ikaitwa TASHRIF. Nimeona niwakumbushe maana wengi wamesahau. Tujifunze kupitia kisa hiki ili kuepusha ajali nyingine za aina hii.!