Mbeya. Utoaji bure wa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV), matibabu na vipimo, vimeokoa maisha ya wananchi 205,501 katika mikoa minne nchini.
Hayo yameelezwa na mshauri mwandamizi wa kinga kutoka ubalozi wa Marekani nchini, Dk Alick Kayange, katika maadhimisho ya miaka 20 ya utekelezaji wa afua ya kutibu na kupunguza maambukizi ya VVU kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (Pepfar).
Simulizi ya Antony Kyando
Miongoni mwa watu hao, yumo mkazi wa Mbarali mkoani Mbeya, Anthony Kyando (67) anakumbuka miaka 27 ya mateso na mahangaiko aliyoyapitia kusaka ARV baada ya kubaini kuwa ana maambukizi ya VVU mwaka 1996.
Akitoa simulizi ya aliyoyapitia wakati wa maadhimisho ya Pepfar, Kyando, aliyezaliwa wilayani Makete, anasema alifika Rujewa wilayani Mbarali kufanya kazi ya uvuvi ambayo ilimpatia kipato kikubwa hata akajikuta akitumbukia katika maisha ya anasa.
"Kutokana na biashara yangu ya samaki, nilikuwa na akiba benki zaidi ya Sh4 milioni mwaka 1996,” anasema.
"Biashara ilikuwa nzuri, nikaanza kuingia katika makundi. Mwaka 1972 nikaoa mke wa kwanza alinizalia watoto watano. Baadaye nikaoa mke mwingine na hapo ndipo matatizo yalipoanza," anasema.
Kyando anasema mwanzoni mwa mwaka 1990, mkewe wa pili alipata mtoto wa kwanza na mambo hayakwenda vizuri, kwa kuwa pamoja na mwanawe walisumbuliwa na maradhi mara kwa mara.
Anasema miaka michache baadaye alipata tena ujauzito na alipokwenda hospitali ya Ilembula, alifahamishwa kuwa mimba ilitunga nje ya kizazi, hivyo alifanyiwa upasuaji.
Baada ya vipimo zaidi, anasema wataalamu wa afya walimshauri kumuacha mkewe huyo bila kumweleza sababu.
"Miaka ya nyuma walisema tu hivyo, hakukuwa na ile mke ana maambukizi basi wanawapima wote. Nilitii nikamuacha na kuendelea na mke wangu. Nilioa mke wa tatu ambaye baadaye nilifahanishwa kuwa alikuwa na maambukizi, baada ya naye kuanza kuumwa. Baada ya muda afya yangu pia ilianza kutetereka," anasema.
Waganga wa jadi
Kyando anasema kutokana na afya yake kudhoofu, ndugu zake walimshinikiza kuwa amerogwa.
"Tulipiga ramli, tukakamata watu uchawi. Kilichonishangaza walikiri kweli wao ni wachawi lakini hawahusiki na ugonjwa wangu. Wengine wakiwataka waganga wawatoe uchawi kwa kuwa hawaupendi na walipewa na babu na bibi zao," anasema.
Anasema mkewe wa pili alifariki dunia mwaka 1996 na wa tatu bado ni mgonjwa. Watoto wake wanne kati ya 10 pia wamekufa.
Kyando anasema alimchukua mkewe wa kwanza na vyeti vya wake zake wengine wawili na kwenda hospitali kwa vipimo zaidi.
Baada ya vipimo anasema aligundulika kuwa na maambukizi ya VVU, lakini mke wake hakuwa ameambukizwa.
Matumizi ya ARV
Kyando anasema baada ya kupata majibu ya vipimo aliacha kutumia dawa za miti shamba na wakati huo afya yake ilikuwa imedhoofu sana.
"Mwaka 1997 nilimweleza shangazi yangu nina maambukizi ya VVU hivyo wasiendelee kutafuta waganga. Shangazi alinyong'onyea kuliko mimi kwa kuwa nilikuwa msaada kwa familia na hata watoto wake. Nilikuwa nikiwalipia karo za shule,” anasema.
Anasema shangazi alimpigia simu binamu yake aliyekuwa akiishi Morogoro hivyo alikwenda mkoani humo kwa ajili ya kufanya vipimo upya.
Vipimo vilionyesha kuwa ni kweli ana maambukizi, hivyo anasema alizungumza na madaktari waliomsaidia kupata ARV kutoka Afrika Kusini.
Kyando anasema alirejea Rujewa ambako aliendelea na matumizi ya dawa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
"Nilirudi na kufuata masharti. Dawa zilipokuja nilikwenda kuchukua na kuelekezwa namna ya kuzitumia, kwa sehemu kubwa zilijaa virutubisho. Niliendelea hivyo na dawa zilikuwa ghali nikauza kila kitu nikaishiwa,” anasema.
Kutokana na gharama za dawa kuwa kubwa, anasema aliuza mali zake, zikiwamo nyumba tatu, viwanja viwili na ekari sita za mashamba na sasa hana tena uwezo kifedha.
Anasema kupitia shirika lisilo la kiserikali la Shdepha, mwaka 2008 watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi walianza kupatiwa misaada ambayo iliwezesha afya zao kuimarika.
Kyando anasema kupitia shirika hilo pia waliweza kujishughulisha na shughuli za kiuchumi hivyo kujiwezesha kimaisha.
ARV zaingia nchini
Anasema mwaka 2004 hali ilikuwa mbaya zaidi na alianza kukata tamaa kwamba hatapata tena ARV, lakini mwaka 2005 akapata taarifa kwamba dawa hizo zinapatikana mkoani Mbeya na zinatolewa bila malipo.
"Ni kauli iliyonipa matumaini makubwa. Nikaenda Mbeya, mimi ni miongoni mwa watu wa kwanza kusajiliwa na kuanzishiwa dawa baada ya vipimo. Baada ya muda tukaona Mbeya ni mbali nikaomba wasogeze huduma Rujewa,” anasema.
Anasema alipatiwa maelekezo kwamba iwapo watu wanaohitaji huduma hiyo wangefika 50 basi huduma ingepelekwa Rujewa.
Kyando anasema akiwa Rujewa alijitangaza kuwa na maambukizi ya VVU na anatumia ARV. Anasema wengine walijitokeza na walipofika 50 huduma ilipelekwa mwaka 2007.
Anasema kwa kushirikiana na wenzake waliendelea kutoa elimu kwa wananchi wilayani Mbarali.
Kyando anasema kutokana na dawa alizokuwa akitumia tangu mwaka 1997 afya yake iliimarika, lakini alishuhudia watu wengine wakinyanyapaliwa na baadhi kutengwa na familia zao.
"Watu walitengwa, changamoto niliyokutana nayo kwanza ni kuwa hawakuamini kama nina maambukizi, waliamini mwenye virusi lazima akonde sana, aharishe na kutapika. Nilishuhudia wakiwa wametengwa kwenye ‘vihenge '(vibanda vya kutunza mazao) na wanasuburi wafe wazikwe," anasema.
Anaishukuru Serikali kwa kushirikiana na Marekani kupitia mradi wa Pepfar kwa kuwawezesha kupata ARV.
"Nawashukuru sana kwa maana huduma ya ARV imekuja wakati nimeishiwa kabisa fedha na nisingeweza tena kuishi. Miaka hii 20 nimeishi kwa dawa za Pepfar, wenzangu ambao walishakata tamaa walifariki dunia lakini mimi naishi mpaka leo," anasema.
"Mke wangu wa kwanza baadaye alipata maambukizi na alifariki kwa kuwa kuna ndugu yangu alimdanganya kwamba angefanyiwa maombi hivyo aache kutumia dawa, kweli aliziacha," anasema.
Aoa tena
Kyando anasema mwaka 2017 alioa mke ambaye hakuwa na maambukizi ya VVU na wana watoto wawili ambao nao hawana maambukizi.
Garasi Meru (35), mke wa Kyando anasema alifikia uamuzi wa kuolewa naye baada ya kufanya kazi za ndani nyumbani kwake kwa kipindi cha miaka kadhaa.
"Nimezaliwa Mbozi. Nilikuja hapa kutafuta maisha nikaishia kufanya kazi za ndani nyumbani kwake nikilea watoto maana waliachwa wadogo. Baadaye nikaridhia kuolewa naye, japokuwa nilipata vitisho vingi kwamba huyu mtu mgonjwa, nilipomuuliza alikiri tukapima na akanifahamisha kwamba nipo salama na sitaambukizwa," anasema.
Mshauri mwandamizi wa kinga kutoka ubalozi wa Marekani, Dk Kayange anasema kwa kipindi cha miaka 20 mradi wa Pepfar umefanya vizuri.
Anasema wanahakikisha vipimo vya VVU na ARV vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Dk Kayange anasema katika kuboresha huduma Serikali ya Marekani imewekeza maabara nchi nzima za kupima wingi wa virusi.
Maabara hizo anasema zinawezesha kupima wingi wa virusi kwa wagonjwa wanaopatikana na maambukizi ya VVU na walioingizwa kwenye mpango wa kutumia dawa za kufubaza virusi .
“Serikali ya Tanzania kwa kushiriki na Marekani imehakikisha hakuna mahali huduma inakosekana, hususan upatikanaji wa dawa na vipimo vya uhakika. Pia kuna maabara za kisasa na wataalamu wa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa uhakika.
"Kama mlivyoona ushuhuda wa wanandoa hawa, wameweza kuendelea kuishi maisha mazuri kutokana na kufuata maelekezo ya matumizi ya dawa kwa mwenza wake lakini mwanamke anaishi bila kuwa na VVU na watoto wakiwa na afya njema," anasema.
Dk Kayange anasema mradi wa Pepfar umeleta mabadiliko makubwa ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa mama kwenda kwa mtoto endapo matumizi ya dawa yanakuwa sahihi, ikiwamo kwa mtu mwenye VVU kutomwambukiza mwenza wake baada ya kupata dawa kinga.
Anasema tangu mwaka 2017 katika mikoa ya nyanda za juu kusini ya Mbeya, Katavi, Songwe na Rukwa watu zaidi ya milioni 3.9 walifikiwa na mradi wa Pepfar.
Dk Kayange alisema tangu kuanza kwa Pepfar miaka 20 iliyopita nchini, Dola za Marekani 6.6 bilioni (Sh15.6 trilioni) zimetumika Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, wanaopatiwa ARV nchini ni watu zaidi ya milioni 1.61.
Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk Anath Rwebembera anasema Serikali inagharimia huduma hiyo kwa Dola za Marekani 330.56 milioni, sawa na Sh778.5 bilioni kila mwaka.