Ni nadra kusikia jambo hili likizingumzwa na wanasiasa na hata viongozi wa serikali, lakini ni kweli kwamba miaka 1980, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipendekeza kuwe na Sera ya Watu.
Katika sera hiyo, Mwalimu Nyerere alitaka kuwekwe masharti kwamba kila familia isiwe na zaidi ya watoto wanne. Sera hiyo ilipingwa vikali na viongozi wa dini, akiamo Dk. Dk. Wilbroad Slaa, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Kwenye ukurasa wa 57 wa kitabu kinachozungumzia maisha yake, alichokipa jina la 'NYUMA YA PAZIA', Dk. Slaa anaeleza namna alivyoingia katika msuguano na Mwalimu Nyerere wakati wa utumishi wake wa kanisa. Hiyo ni baada ya kumpinga Baba wa Taifa, kuhusu Sera hiyo ya Watu
Dk. Slaa anaweka wazi kuwa mazungumzo yake na Mwalimu Nyerere kipindi hicho yalikuwa yanafanyika majira ya saa 6-7 usiku na anaamini 'hakushughulikiwa' kwa kupinga sera hiyo kwa kuwa hata viongozi wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) waliipinga.
Hata hivyo, Dk. Slaa anaeleza kuwa msimamo wake huo ulifanya Mwalimu Nyerere atume ndege maalum kumfuata Musoma kwenda Dodoma Januari 6, 1989, kujieleza mbele ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwanini TEC ilipinga sera hiyo.
Wiki hii, baada ya miaka 34 kupita, Nipashe katika mazungumzo maalum na Dk. Slaa inahoji kama mwanasiasa huyo amebadili msimamo wake na kuunga mkono sera hiyo ya Mwalimu Nyerere.
Dk. Slaa ana majibu katika hilo, akieleza: "...hoja yangu ya msingi ni kwamba udhibiti wa ongezeko la watu ni uamuzi kati ya mwanamume na mwanamke. Si uamuzi wa serikali. Kumbuka wakati tunajadili hilo, China walikuja na sera kwamba akizaliwa mtoto wa kike anauawa.
"Kwanza (sera) ilikuwa mtoto mmoja kwa familia. Na akizaliwa wa kike anauawa kwa sababu anakwenda kutuzalia watoto wengine. Je, hiyo ni haki? Kwa hiyo Mwalimu wakati ule alikuja na sera za Urusi na China za ujamaa.
Kumbuka wakati huo mwalimu alikuwa amevutiwa na ujamaa, hivyo akaja na sera ya watoto wanne tu. Sasa mtanzania unamwambia watoto wanne. 'Mungu amenipa utajiri wa ng’ombe 1,000 halafu unasema watoto mwisho wanne tu!'
Mungu amekupa utajiri ule wa ng’ombe na watoto kwa sababu una uwezo wa kuwatunza. Ni tofauti na mtu mwingine katika kijiji kile pale - hana shamba, ikizidi sana ana robo ekari, yeye huyo sasa anapaswa kutumia busara yake aliyopewa na Mungu kwamba 'nitawalishaje nitakapokuwa na watoto zaidi?'
"Kwa bahati mbaya wa Afrika tulikuwa na imani kuwa kila mtoto anakuja na neema yake, jambo ambalo si kweli, ndiyo maana wengine wanakosa nguo lakini huo ni mpango wa baba na mama namna gani wapate mtoto wao."
SWALI: Sasa tunashuhudia ongezeko kubwa la watu nchini. Tufanye nini kulikabili kama hatuitaki hii sera ya Mwalimu?
DK. SLAA: Elimu tu itolewe kwa wingi. Yeyote ambaye amesoma masuala ya population growth (ongezeko la idadi ya watu) yanasema hivi - ukimpeleka binti darasa la kwanza mpaka la saba, anapunguza idadi ya watoto wa kuzaa. Yeye mwenyewe tu hata kama mwanamume anataka.
Atakudanganya atakwenda kupiga zile sindano, hakuambii. Nina uhakika humu wengine mnapiga hizo sindano (waandishi wanawake). Je, huwa mnawaambia waume zenu?
Hizo zipo. Wanajua lakini hawatungiwi sheria. Serikali ikishaingia katika mambo hayo ni serikali ya kidikteta. Mambo ya uzazi mwachie mtu mwenyewe. Mungu ametupa akili, busara na hekima ili tujiongoze kama binadamu.
SWALI: Utawala wa Hayati Dk. John Magufuli ambao wewe ulikuwa balozi wake, unanyooshewa kidole kwa kubana demokrasia. Kwanini umekuwa kimya katika hili?
DK. SLAA: Wakati huo Dk. Slaa alikuwa nani? Je, majukumu ya balozi ni nini? Ungeniambia labda 'Dk. Slaa ulipokuwa Sweden', hukutekeleza majukumu yako ya kibalozi.
Wakati huo mimi sihusiki na siasa ila unaweza kuniuliza niliwezaje kuimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi nilizokuwa ninaziwakilisha na picha unaziona hapo ukutani. Jinsi nilivyoleta wafanyabiashara, kwa sababu ndiyo ilikuwa kazi yangu lakini sio siasa.
Hoja za kwenye mitandao huwa hazinisumbui. Mimi huwa ninasema Magufuli ni binadamu. Tutambue ana mabaya yake na mema yake. Kuna vitu vizuri alivyofanya. Kwa mfano, hebu nionyeshe hata mtu mmoja aliyewahi kufanya utafiti kuwa Magufuli hiki aliiba. Yupo?
Ni maneno na hisia. Sasa, kwa mtu kama mimi, ambaye nimeshughulika na masuala ya ufisadi ambao unakwenda mpaka katika kabati ya serikali unanyofolewa karatasi kule ndani, unaonyeshwa kuwa huu ni wizi! Mimi kelele za mtaani hazinisumbui.
Tatizo kubwa sana la Magufuli ambalo mimi ninaliona, ni kuminya demokrasia. Kumbuka mwaka 2015 mimi nilisimama jukwaani kama mnakumbuka, kabla sijaondoka.
Niliondoka Septemba Mosi, lakini baadaye nilirudi kwa sababu kulikuwa na kitengo cha CCBRT tulikuwa tunakifungua na JK (Rais Jakaya Kikwete). Kwa hiyo, nikarudi Oktoba, nilikuwa katika kipindi kimoja cha chombo cha habari, nikaulizwa nitoe tathmini na nilisema kauli moja kwamba kama ingekuwa uchaguzi ni kitu ambacho kina gia ya reverse kama gari, lakini uchaguzi sio hivyo, hatua moja ikishapita imepita.
Sasa nikasema katika hatua hiyo kwa kuwa hatuwezi kurudi nyuma, nikasema mimi hapa sioni anayefaa katika wote waliokuwa wanagombea. Ingekuwa inawezekana tufute tuanze upya, lakini kwa kuwa hapakuwa na uwezekano kwa sasa tulionao kati ya Lowassa na Magufuli, maana ndiyo walikuwa wagombea wakubwa, mimi ninaona mwenye dhambi kidogo ni Magufuli na niliyasema makosa yake ikiwamo kutoa nyumba ya serikali kwa watu wasiostahili.
Katika suala la mikutano ya hadhara, Magufuli alidanganywa na mawaziri wake waliomweleza kuwa uchaguzi huko Marekani ukiisha, siasa zinaendelea bungeni na nilikwenda nikawahoji hao mawaziri wakaniambia 'sasa balozi nani wa kumwambia tena Rais arekebishe kauli yake kwamba tulichomwambia hakikuwa sahihi?'
Wakaniambia cha kufanya ikifika Januari 2020, watabadilisha ile sheria lakini ilipofika hawakubadilisha. Magufuli aliibeba kwa sababu inamfaa kisiasa lakini waliomwandalia ni mawaziri wake ambao ni wanasheria na walikiri kwamba wao ndiyo waliompotosha Rais.
Suala lingine la kuhusu ndege ambalo watu wanasema amepiga, ukimuuliza mtu amepiga ngapi, hajui! Sisi enzi zetu tulikuwa tunafuatilia kwa kina. Tulimbana Mwandosya akiwa Waziri wa Mawasiliano, mimi na Hamad Rashid tukajifanya wapigania uhuru wa Congo, tukaandika email Marekani kiwandani kufuatilia bei ya ndege ya Rais wakati huo, ndani ya dakika mbili kampuni iliyowauzia ndege ikatupa jibu la bei halisi ya ndege hiyo.
Tukamwabia waziri umetudanganya. Leo kuna anayefanya hivyo? Tukafanya hivyo, kupata bei halisi ili kumkosoe waziri ambaye ndani ya Bunge anaonyesha bei yake na sisi tukiwa na bei halisi.
Ingekuwa kuna mtanzania amefuatilia kwa kiwango hicho, hapo ningeelewa na hayo makosa anayafanya hata Lissu leo na nilimwandikia meseji juzi kwa mliouliza kuwa tunawasiliana. Tunawasiliana.
SWALI: Zipo taarifa kwamba hauko sawa na familia yako. Kuna ukweli upi katika hili daktari?
DK. SLAA: Nina watoto wawili na mama wa kwanza ambaye hatujafunga ndoa, Rose Kamili, ambao leo ni watu wazima. Baadaye nikafunga ndoa kule Canada na Josephine lakini tulikuwa tumeshapata mtoto wetu tukiwa huku na huyo mama sasa ambaye tulifunga ndoa (Josephine) tuna watoto watatu na Rose (watoto) wawili.
Hao wa Josephine wote wako Canada kwa sababu wanasoma. Mimi nilipokwenda Sweden, sikuweza kuwahamisha kwa sababu mifumo ya elimu inatofautiana na unajua katika kazi ya ubalozi, leo upo hapa miaka miwili kesho miaka mitatu uko kwingine. Sasa Sweden, kwa mfano, lazima kwanza ujifunze lugha yao mwaka mzima.