Spika Dk Tulia 'Tozo za mkongo wa Taifa ni mzigo kwa wananchi'

Spika Dk Tulia 'Tozo za mkongo wa Taifa ni mzigo kwa wananchi'

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema tozo kubwa zinazotozwa mkongo wa taifa unapopita kwenye hifadhi za barabara zimekuwa zikisababisha gharama kubwa za huduma kwa wananchi.

Dk Tulia amesema Bunge liko tayari kulifanyia kazi jambo hilo ikiwa serikali itakuwa na utayari wa kupunguza tozo hizo ili wananchi ambao ni walaji wa mwisho wapate huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu.

Akizungumza jana Mei 13, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa minara ya simu, Dk Tulia amesema gharama za kupeleka mkongo wa Taifa sehemu mbalimbali za nchi zinakuwa ni ghali pale mkongo unapopita kwenye hifadhi za barabara.

“Ukiangalia zile bei, ikipita kwenye mtandao wa maji, bei ni ndogo, ikipita kwenye mtandao wa simu bei ni ndogo lakini ukipita kwenye mtandao wa barabara inakuwa ni zaidi ya Dola 1000, hiyo inakuwa ni bei ghali, kwa hiyo watoa huduma nao wanataka kufidia ile gharama.

“Sisi kama Bunge tuko tayari kulifanyia kazi hilo ikiwa Serikali itakuwa na utayari wa kuipunguza tozo hiyo ili kupunguza gharama za mawasiliano ziweze kufika kwa urahisi vijijini,” amesema Spika Dk Tulia.

Amebainisha kwamba yapo malalamiko ya wananchi kwamba sekta ya mawasiliano ni ghali, matumizi ya simu janja na mabando ni ghali. Amesisitiza kwamba huo ughali utakwenda kupungua kupitia minara hiyo inayopelekwa maeneo ya vijijini.

“Kama ikipelekwa kule vijijini na bei ikawa haijapungua, uwekezaji huu unaofanywa na serikali unaweza kuonekana hauna tija katika kipindi kifupi lakini tukiunganisha hii minara inayokwenda vijijini na sekta ya nishati,” amesema Spika Dk Tulia.

Akizungumzia tozo hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema tozo hiyo iliwekwa miaka ya nyuma wakati huduma ya mkongo haikuwa ya lazima, lakini kwa sababu sasa ni wa lazima, Serikali inakwenda kuliangalia hilo ili wananchi wasipate gharama kubwa kwenye mawasiliano.

“Ili tushushe gharama na watu wetu wakatumie vizuri huduma hii kule vijijini, lazima Serikali tuliangalie hili,” amesema Rais Samia wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye hafla hiyo jijini Dodoma.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad