Story ya Kifo cha MC Joel Inaonesha “Aliwaza, Akapanga, Akatekeleza”.




MAJENGO matatu jirani yanaitwa “Derm". Fupi kongwe ni Derm House. La pili ni Derm Complex. Haya yapo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Nyuma ya Derm House ni Derm Plaza ambalo ni refu kuliko mengine yenye ubini wa “Derm". Top floor ya Derm Plaza kuna msikiti.

Waislamu wana vipindi vitano vya sala kwa siku. Magharibi, Isha, Subuhi (Fajri), Dhuhuri na Laasir.

Joel Misesemo ni Mkristo. Anaendesha gari kutoka alikotoka hadi Derm Plaza. Gari lipo salama. Anapaki vizuri. Hana papara.

Anashuka. Anafunga milango ya gari vema. Anaelekea Derm Plaza, mlinzi anamhoji aendako. Anajibu; “Naenda Masjid.”

Muda ni saa 11 asubuhi. Ni ‘wakti’ sahihi wa Sala ya Fajri. Jengo lina Msikiti. Unamtilia shaka mtu anakwenda kutekeleza wito wa Mola wake? Mlinzi akamtakia “ibada njema".

Joel au MC Joe ni Mkristo. Chukua mambo mawili; mosi, anajua vizuri kuwa top floor ya Derm Plaza ni msikitini. Pili, anafahamu saa 11 ni muda wa sala kwa Waislam.

Muda mwingi anazungumza na simu. Matokeo ya baadaye yanaleta nadharia; alizuga kuongea na simu kukwepa watu mpaka atimize lengo lake; kujitoa uhai.

“Suicidal Ideation” – “Fikra za Kujiua" ni ugonjwa wa akili wenye matawi mawili; Mosi, Active suicidal thoughts - mwenye kuwaza na kupanga utekelezaji.

Pili, Passive suicidal thoughts – anawaza kujiua, hajui aanzie wapi.

Story ya kifo cha Joel inaonesha “aliwaza, akapanga, akatekeleza”.

Aliwaza kujiua; inawezekana alipoteza matumaini au alitendwa, akashindwa kuhimili maumivu. Pengine alijiona ana hatia au alijikuta katikati ya aibu iliyomwelemea. Aliona maisha hayana maana.

Alipanga kujiua; alichagua kifo cha kujirusha ghorofani.

Jengo gani rahisi kwake kujiua? Inawezekana alifanya utafiti, akabaini Derm Plaza linafaa kutimiza azma yake. Saa 11 asubuhi ingekuwa muda mzuri, kusingekuwa na hekaheka za watu na angedanganya anaelekea msikitini.

Baada ya mchoro kukamilika, alitekeleza na kujirudisha kwa Mungu kabla ya wakati.

Umekuja duniani kuishi. Walimwengu watakulazimisha uone maisha hayana maana.

Yakikufika. Usimtazame yeyote isipokuwa Mungu. Usiwaze watu watakuchukuliaje. Wengi hujiua sababu ya watu wengine.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad