Chama cha upinzani Chadema mkoani Mbeya imeanza mikutano ya hadhara leo katika Kata ya Nzovwe, huku aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo, Joseph Mbilinyi 'Sugu' akitangaza kumtaka Mbunge wa sasa Dk Tulia Akson, katika kinyang’anyiro hicho.
Katika mfululizo wa mikutano hiyo ambayo imeanzia kata ya Uyole, Sugu ndiye anaonekana kuwa kinara huku akipewa hamasa na viongozi wengine wa chama hicho mkoani humo.
"Tunakutaka Tulia, tunakutaka Tulia, tunakutaka Tulia" ni kauli Sugu akielezea mjadala ulioibuka juu ya kugawanya kwa jimbo Mbeya mjini, mapendekezo yanayosemekana kuwasiliwa na Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sugu ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 10, (2010-20) kabla ya uchaguzi Mkuu uliopita kuchukuliwa na Dk Tulia Ackson ambaye pia ni spika wa bunge kwa sasa.
Akizungumza leo Alhamisi Mei 11 kwenye mkutano huo Sugu amesema alisikia hoja hiyo lakini hakuwahi kulielezea popote akisisitiza kuwa yeye analitaka Jimbo la Mbeya mjini.
Amesema yeye akiwa Mbunge aliweza kuzihudumia Kata zote 36 za Jimbo hilo, lakini anashangaa hoja ya kuligawa na kwamba vyovyote iwavyo anamtaka Dk Tulia Ackson popote.
"Nashangaa kwanini huyu spika anapaniki tu, mimi sijaongea chochote tayari ameanza kuzungumzia hili jambo, sasa nasema hivi tukutane 2025 kwani aliyemuweka bungeni kwa sasa hayupo tena"
"Anatuletea muziki na wasanii hivi hii Mbeya ya sasa inataka muziki na wasanii? Muziki ulitokea hapa na mimi ndiye nilitambulisha soko la muziki hadi nje ya nchi, nasema tunakutaka Tulia tunakutaka Tulia tunakutaka Tulia," amesema Sugu.
Ameongeza kuwa alipopata ubunge alikuta Jimbo likiwa na kilomita tisa za lami, lakini hadi anaondoka aliacha kilomita 87 lakini kwa sasa hajui kama kuna nyongeza zaidi licha ya mpango wa serikali kujenga njia nne.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama hicho mkoani humo, Joseph Mwasote amewaomba wananchi kila mmoja kuzungumza na familia yake ili aliyekamilisha vigezo vya kupiga kura kujiandaa kujiandikisha kwenye daftali la wapiga kura.
Ameongeza kuwa katika hoja ya kugawa majimbo, hata yeye anajipanga kufanya tathmini ili jimbo la Mbeya vijijini nalo ligawanywe.
"Leo tunaanza upya safari yetu baada ya kipindi kigumu na kirefu tulichopitia, tunataka katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, hatutaki tena wabunge, madiwani wa promosheni, kazi tunaenda kuiwasha kwenye serikali za mitaa mwakani," amesema Mwasote.
Naye mwenyekiti mstaafu wa Chama hicho, John Mwambigija amewataka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa kuweka usawa kwenye ajira za muda mfupi na kudumu akisema kuwa Chadema kinao vijana wengi wasomi kila idara ikiwamo uhandisi.
"Tunatarajia kuwasilisha majina ya vijana 500 tutengeneze mgawanyo ili haki itendeke sehemu zote, tumeanza na 'operesheni chakaza' Mkoa mzima kukiwasha ili Mbeya itulie, wale waliopo bungeni hawawezi kuhoji kwakuwa waliingia kwa hisani hawakupigiwa kura"
"Zipo pesa za wananchi zikiwamo za viwanja Kata ya Iduda, ambazo zimetumika kununulia magari pale Halmashauri ya Jiji lazima tujue hatma yake, uchaguzi ujao hatutaki viongozi wa promosheni" amesema Mwambigija.