Tanesco yataja chanzo umeme kukatika bungeni



Dar/Dodoma. Baada ya umeme kuzimika bungeni mara kadhaa wakati wa kikao cha leo Mei 15, 2023, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limejitokeza na kufafanua kwamba kukatika huko kwa umeme hakuhusiani na laini ya Tanesco inayopeleka umeme katika ukumbi huo.

 Leo baada ya kipindi cha maswali na majibu kwisha, Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi alisimama kuchangia kuhusu hotuba ya Waziri wa Afya ambayo iliwasilishwa mwishoni mwa wiki.

Wakati akizungumza, umeme ukakatika na ndani ya dakika tatu umeme ulikatika kama mara mbili, wabunge wakabaki wametulia wakisubiri urudi. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuona hivyo akaamua kuahirisha shughuli za Bunge.

Akizungumzia kuhusu kukatika kwa umeme bungeni, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Martin Mwambene amesema laini ya umeme ya Bunge inaangaliwa kwa makini kwa kuwa hiyo ni taasisi nyeti na inapewa kipaumbele kama vile hospitali.


“Tumeona hiyo taarifa kwamba kuna tatizo la umeme lakini tunaamini tatizo halitoki kwetu na laini yetu iko intact (haijaharibika),” amesema.

Amesema watu wamekuwa wakihusisha kila kukatika kwa umeme na Tanesco, jambo ambalo amesema siyo kweli kwa sababu wajibu wa Tanesco unaishia kwenye mita, lakini ukiingia ndani, ni eneo linalomhusu mteja.

“Tatizo ambalo limepatikana hapo (bungeni) halihusiani na laini yetu kutoka au vinginevyo na kuzima na kuwaka ni dalili pia ya shot, sasa shot inaweza kuwa ndani ya majengo yenyewe au vinginevyo,” amesema Mwambene.


Chanzo cha kuaminika kutoka Bungeni, kimeiambia Mwananchi Digital kuwa mafundi wa Tamesa wamebainisha kuwa kuwa tatizo lilikuwa ni ‘circuit breaker’ iliyokuwa inatumika kuwa na mfumo wa kizamani.

“Baada ya mafundi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kubadili earth leakage circuit breaker, na kufunga miniature circuit breaker ya kisasa; sasa umeme umerejea mjengoni hapo,” kilisema chanzo hiko.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad