THBUB yajitosa Kuchunguza Kifo Tata cha Mwanafunzi UDOM



Kufuatia utata wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdallah, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeazimia kufanya uchunguzi huru kwa madhumuni ya kubaini ukweli kuhusu tukio hilo.


Marehemu Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii, ambapo kifo chake kimejaa utata.


Pia, ndugu wa marehemu kupia Baba mkubwa Ali Selemani wametilia shaka uharaka wa mazishi yake yaliyofanyika Iramba mkoani Singida na kuibua maswali ambayo majibu yake ni magumu.


Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatano,Mei 10,2023 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema wanatambua uwepo wa vyombo vinavyoshughulikia masuala ya haki jinai hususani Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.


Jaji Mwaimu amesema kwa kutambua hivyo tume inavipa heshima vyombo hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake.


Amesema kunapotokea mashaka ya haki kutotendeka tume inayo mamlaka ya kufanya uchunguzi wa jambo hilo kwa mujibu wa katiba na sheria ya tume kwa kuwa inayojukumu la kutetea na kulinda haki za binadamu nchini.


Jaji huyo Mstaafu amesema kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) cha Sheria za haki za binadamu na utawala bora sura ya 391 tume inayo mamlaka ya kuanzisha uchunguzi wenyewe juu ya malalamiko yanayoashiria uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.


“Kwa muktadha huo tume imeazimia kufanya uchunguzi wake huru kwa madhumuni ya kubaini ukweli kuhusu matukio hayo,” amesema mwenyekiti huyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad