MWANZA. KITAYOSCE imepanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship nyuma ya vinara JKT Tanzania, lakini sasa inabidi isikilizie kutokana na klabu ya Pamba kuiburuza Shirikisho la Kimataifa ya Soka (FIFA).
Timu hiyo inayoelezwa inajiandaa kuanza kutumia jina ya Tabora United baada ya kubadilishwa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi, imeburuzwa FIFA na uongozi wa Pamba kutokana na kesi iliyompa kifungo cha maisha Mwenyekiti wa Kitayosce, Yusuf Kitumbo na Kocha Ulimboka Mwakingwe.
Pamba iliwasilisha FIFA ombi la kuomba ufafanuzi wa maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) juu ya tuhuma sakata la upangaji matokeo zilizowahukumu wawili hao na ombi hilo limewasilishwa Mei 16, mwaka huu saa 10:56 jioni ikiomba uchunguzi wa sakata hilo, tayari FIFA imeshaijibu barua yao likiahidi kutoa taarifa zaidi kutokana na jambo hilo.
Ofisa Habari wa Pamba, Moses William alisema wanachokilalamikia ni kutochukuliwa kwa hatua zozote za kikanuni baada ya Kitayosce kuchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Pia wanalalamikia itayosce kutochukuliwa hatua licha ya mmiliki na mwenyekiti wake kufungiwa maisha kutojihusisha na soka baada ya kubainika kujihusisha na upangaji matokeo.
“Maamuzi yaliyotoka mpaka sasa kwenye mamlaka zetu za soka hatujaridhishwa nayo kwani walalamikiwa walitakiwa kuadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za mashindano. Tunachosubiri sasa ni maamuzi kutoka FIFA kwa sababu tayari wameshatujibu kuwa wamepokea malalamiko yetu na wanayafanyia kazi," alisema Moses.
Hata hivyo, mjumbe wa Kamati ya mashindano Pamba, Alhaji Majogoro alisema wanachoomba ni ufafanuzi wa upangaji matokeo na ukakasi wa kiutendaji unaozunguka sakata hilo, kwani wana nia njema ya kuhakikisha wanaipa thamani stahiki Ligi ya Championship.