Tishio umwagaji damu lamshtua Mkuu wa Wilaya



TISHIO la umwagaji damu lililotolewa na familia mbili za kifugaji katika Kijiji cha Lendikinya, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, limemshtua Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Nassari.

Amesema kutokana na tishio hilo, amelazimika kuingilia kati kutafuta amani baina ya pande mbili zinazozozana kuhusu uhalali wa umiliki wa ardhi.

Anayedaiwa kumiliki ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 26 kwa mujibu wa sheria za ardhi ni Nakudana Mungaya, lakini familia mbili za kifugaji zinazowahusisha, Yamat Mbaranot na Mbarnot Marmalu, zinadai ardhi hiyo ni mali yao na wanaimiliki kihalali.

Akizungumzia mgogoro huo mwishoni mwa wiki, Nassari, alisema amelazimika kuingilia kati mgogoro huo kutokana na kutishia amani ya wakazi Lendikinya pamoja na kuhatarisha maisha ya familia zinazogombana.

“Walikuwa na kesi katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya na iliamuliwa kwa Nakudana Mungaya kupewa haki ya umiliki wa ardhi hiyo. Sasa baada ya uamuzi huo kutolewa, walalamikiwa Yamat Mbaranot na Mbarnot Marmalu, hawakuridhika na uamuzi uliompa haki Nakudana.


“Kutokana na kutokubaliana na uamuzi huo wa baraza, Yamat Mbaranot na Mbarnot Marmalu, waliendelea na msimamo wao wa kugomea kuachia ardhi hiyo na kutishia kumwaga damu. Ndiyo maana nikaenda eneo husika lenye mgogoro na kuagiza wote wafike ofisini kwangu tulimalize hili sakata kwa amani.”

Nakudana, alipewa ushindi katika shauri namba 125 la mwaka 2007 lililoamliwa na baraza hilo. Alipata ushindi huo uliotolewa na Mwenyekiti wa baraza hilo, Fadhili Mdachi, aliyeamuru eneo lenye shamba lenye mgogoro lenye ukubwa wa ekari 26 lililopo Moranda katika kijiji hicho kuwa ni mali ya mlalamikaji.

Kabla ya Nassari kuingilia kati mgogoro huo, Nakudana, alilalamika akidai kutishiwa maisha na wanakijiji wenzake walioungana na walalamikiwa katika mgogoro huo.


Kutokana na mgogoro huo, Nakudana, amemwomba Mkuu wa Wilaya ya Monduli, kuipa ushirikiano kampuni ya udalali ya Regiz Co. Ltd ya Jiji la Arusha kutekeleza amri halali ya baraza hilo ya kuwaondoa kwenye ardhi yake walalamikiwa walioshindwa kesi hiyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad