TUCTA yamtwisha zigo Rais Samia



Katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi duniani (Mei Mosi), Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limezitaja hoja ambazo wanatarajia kuzifikisha kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan zikiwemo nyongeza ya mishahara, malimbikizo ya madeni, mazingira bora ya kazi na mikataba ya ajira.


Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2023 mjini Morogoro na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi ambapo amesema licha ya madai hayo kuwasilishwa kwenye Mei Mosi ya mwaka jana na Serikali kuyatolea tamko lakini bado wapo waajiri wachache ambao hawajatekeleza hasa madai ya nyongeza ya mishahara. Amesema miongoni mwa madai yaliyofanywa kazi ni pamoja na ya malipo kwa wafanyakazi walioondolewa kazini kutokana na vyeti feki na wale waliokuwa na vyeti vya darasa la saba.


Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani, kitaifa yatafanyika kesho Mei 1, 2023 mkoani Morogoro yenye kauli mbiu inayosema "Mishahara bora na ajira ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi" Pamoja na mambo mengine Nyamhokya akizungumzia suala la baadhi ya viongozi wa TUCTA na vyama vya wafanyakazi kuwa makada wa vyama vya siasa amesema suala la siasa kwenye moyo wa mtu haliwezi kuondolewa isipokuwa kinachokatazwa kwa viongozi hao ni kuleta siasa kwenye masuala ya wafanyakazi. Kuhusu utulivu uliopo kwa sasa ndani ya TUCTA, Nyamhokya amesema jambo hilo limetokana na kukaa meza moja na Serikali pamoja na waajiri na kuruhusu majadiliano kwa njia ya mazungumzo na kufikia makubaliano. "Wananchi wamezoea vibaya, wamezoea TUCTA yenye maandamano kila siku, sasa hivi TUCTA tunamaliza matatizo yetu kwa njia ya mazungumzo na sio maandamano na migomo," amesema Nyamhokya Mmezoea vibaya. Awali Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amekagua uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro utakaotumika katika maadhimisho hayo ya Mei Mosi kitaifa na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa, wabunge, mawaziri, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na kamati ya maandalizi ya sherehe hizo. Majaliwa amesema kuwa kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na maandalizi yaliyofanyika na kuwaomba wafanyakazi wa mkoani Morogoro na mikoa mingine kujitokeza kwa wingi kuujaza uwanja huo. "Kuhusu mvua hizi zinazoendelea kunyesha hapa Morogoro naamini wapo wazee wa mila watafanya mambo mvua hizi kwa kesho zitatulia," amesema Majaliwa

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad