Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Tundu Lissu amesema, maridhiano pekee ni kupatikana kwa Katiba mpya, kabla ya uchaguzi mkuu 2025 kwani na isipopatikana itakuwa imekula kwao.
Amesema endapo watakubali kusubiri hadi baada ya uchaguzi mkuu ndio Katiba ipatikane, wataibiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
Desemba 2022, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ya mchakato wa maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Samia kwa mara ya kwanza, alikutana na Mbowe Machi 4, 2022, Ikulu ya Dar es Salaam saa chache baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani alikokaa kwa takriban miezi tisa kwa tuhuma za ugaidi.
Hata hivyo, kikao chao hicho kilifungua milango ya vikao vingine baina ya viongozi wa vyama hivyo vilivyoendelea mara kadhaa, kuyasaka maridhiano ya kisiasa.
Kauli hiyo ya Lissu ambayo ameitoa leo Jumatamo Mei 10, 2023 mkoani Singida, ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya hadhara aliyoianza hivi karibuni mkoa wa Morogoro.
“Kuna maneno mengi ya upatanisho, na maridhiano pekee ni upatikananji wa Katiba mpya, tusipokuwa na katiba mpya tumeliwa, maridhiano ambayo hayana ukweli, watu waliumizwa sana lakini hawajaambiwa kwanini waliumizwa, wala nani aliyeamuru waumizwe wala kufidiwa,”amesema Lissu.
Alisema hata kwa watu wanaofuata dini hawawezi kusamehewa bila kufuata maungamo, kwani kuna watu wameiba kwa miaka mingi ambao wanazungumzia maridhiano.
“Hakuna mtu anayechukia watu kupatanishwa lakini hakuna upatanisho bila kweli, hakuna upatanisho bila haki, wapo watu wetu waliopotea wengine wameumizwa na kuuwawa,” amehoji Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema Tanzania Bara.
Akizungumzia mchakato wa Katiba mpya Lissu alisema, mchakato wa Katiba ni wa watu wote na kwamba ni kwa katiba hiyo wananchi wanapata chakula na mahitaji mengine muhimu lakini pia ni kwa katiba hiyo uamuzi wa nani atawale huwa dhahiri.
Alisema tangu nchi imepata uhuru kwa mara ya kwanza kuna wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa ambao hawakutokana na kura za wananchi.
“Fikiria kama hukuwachagua, utakapovamiwa kuna wakuwatetea? Kwenye udiwani hakuna hata mmoja aliyechaguliwa, wako bungeni na kwenye halmashauri, mkiumizwa kuna wakuwatetea,”amehoji Lissu.
Lissu ambaye amewahi kuwa mbunge wa Singida Mashariki, alisema kwa hali hiyo fedha zitaliwa na hakuna wa kuwatetea.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa Kanda ya Kati (Chadema) Emmanuel Masonga amesema suala la vijana kubeti, linawafanya maskini badala ya kufikiria kuwekeza kwenye mashamba.
Amesema Serikali imeshindwa kuwasaidia ili wawekeze kwenye kilimo, wamewaacha matokeo yake wameingia kwenye kubeti.
“Mkiendelea kuchagua CCM, nitaendelea kubeti, wabunge wana msemo wao CCM ina wenyewe na wenyewe ndio sisi,”amesema Masonga.